MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa jana amefunga bao lake la tatu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, ingawa timu yake, KRC Genk ilichapwa 4-1 na Salzburg ya Ausrtia katika mchezo wa Kundi E Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
Samatta alifunga bao lake dakika ya 85 hilo la pili kuwafunga Salzburg, kwani hata kwenye mchezo wa kwanza pia Genk ikichapwa 6-2 Septemba 17 Uwanja wa Red Bull Arena, yeye ndiye aliyefunga bao la pili la timu yake.
Bao lingine Samatta amefunga dhidi ya Liverpool Novemba 5 Uwanja wa Anfield kwenye mchezo uliopita na Napoli ambayo itamenyana na Genk katika mchezo wa mwisho Desemba 10 Uwanja wa San Paolo mjini Napoli inabaki kuwa timu pekee ambayo haijafungwa na Mtanzania huyo kwenye kundi lao.
Mabao ya Salzburg jana yalifungwa na Mzambia Patson Daka dakika ya 43, Mjapan Takumi Minamino dakika ya 45, Mkorea Hwang Hee-Chan dakika ya 69 na Mnorway, Erling Haland dakika ya 87.
Bao hilo la tatu katika Ligi ya Mabingwa jana, linamfanya Samatta afikishe jumla ya mabao 70 katika mechi 176 za mashindano yote tangu ajiunge na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 137 akiwa amefunga mabao 53, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja, Ligi ya Mabingwa Ulaya mechi nne na hayo mabao matatu na Europa League mechi 24 na mabao 14.
Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Coucke, Maehle, Dewaest, Lucumi, De Norre, Cuesta, Berge, Hrosovsky/Onuachu dk59, Ito/Hagi dk79, Samatta na Paintsil/Bongonda dk65.
Salzburg; Carlos, A. Ulmer, J. Onguene, M. Wober, R. Kristensen, Z. Junuzovic, D. Szoboszlai/M. Okugawa dk80, E. Mwepu, T. Minamino/A. Vallci dk89, Hwang Hee-Chan na P. Daka/E. Haland dk62.