Mkurugenzi wa Taasisi ya Immacate foundation akizungumza kwenye hafla fupi ya ufunguzi wa ofisi mpya iliyofanyika Machi 18, 2024 Jijini Mwanza
Askofu wa Kanisa la Giligali Eliabu Sentozi (wakwanza Julia) akikata utepe ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa ofisi mpya ya taasisi ya Immacate foundation
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Taasisi ya Immacate Foundation inayojihusisha na kusaidia watoto wenye ulemavu imeendelea kuwapa tabasamu watoto hao kwakuwapa mahitaji muhimu ikiwemo kuwapeleka shule,kuwakatia bima ya afya,kuwanunulia viti mwendo pamoja na mahitaji ya mavazi na chakula ili waweze kutimiza ndoto zao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Immacate foundation Emmanuel Julius wakati alipokuwa akizungumza kwenye hafla fupi ya ufunguzi wa ofisi mpya ya taasisi hiyo iliyofanyika Machi 18, 2024 Jijini Mwanza.
Amesema taasisi hiyo ina watoto 220 ambapo kati yao wapo watoto wamewapeleka shule sanjari na kutoa huduma ya bima ya afya kwa watoto ambao hawajaanza shule ili waweze kupata matibabu kwa uhakika pindi wanapougua.
“Watoto wenye ulemavu wanachangamoto kubwa ya afya hivyo wanapokuwa na bima ya afya inasaidia sana katika kupata matibabu ndio maana taasisi hii imekuwa ikijitahidi sana kuwakatia bima hizo ili ziwasaidie pindi wanapougua”, amesema Julius
Aidha, alieleza kuwa awali bima za afya kwa watoto walikuwa wanachangia elfu 50,400 lakini kwa sasa kila mtoto anachangia 120,000 gharama ambayo ni kubwa ukilinganisha na hali ngumu ya uchumi iliyopo kwenye jamii.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Askofu wa Kanisa la Giligali Eliabu Sentozi, amesema watu wenye maono mbalimbali ya kusaidia jamii wapo wengi ila wanakuwa hawajitokezi,pia ameongeza kuwa anafurahia sana kuwa baba wa watu wenye maono ambao wanamlengo mzuri wa kuisaidia jamii katika nyanja mbalimbali.
“Ukitaka kuishi kwako kuwe na maana ni pale utakapoishi maisha kwaajili ya watu wengine maisha unayoishi kwaajili ya wengine yana maana kubwa sana na hayafi unajikuta umesaidia watu wengi na kurithisha vizazi na vizazi, hivyo jitokezeni muweze kusaidia watu wenye mahitaji mbalimbali na Mungu atawabariki”, amesema Askofu Sentozi