Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) akifafanua jambo kwenye majadiliano ya awali na Ujumbe wa Italia kuhusu Mpango wa Mattei. Pembeni yake ni, Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk, Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Na.Mwaandishi Wetu_ Dar es Salaam
Tanzania na Italia zimeanza kujadili hatua ya awali kuhusu Mpango wa Kimkakati wa nchi ya Italia wa Mattei (Mattei Plan) unaolenga ushirikiano na Afrika kwenye sekta mbalimbali za kipaumbele.
Ujumbe wa serikali ya Tanzania na Italia uliokutana Machi 15, jijini Dar es Salaam umeanisha sekta za kilimo, nishati, elimu, afya na uchumi wa buluu kuwa za kipaumbele kama hatua ya awali kuelekea majadiliano ya kina kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Mattei.
Akizungumza kuhusu wakati wa majadiliano kuhusu mpango huo wa ushirikiano baina ya nchi ya Italia na bara la Afrika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, amesema vipaumbele vilivyobainishwa vinaendana na mahitaji ya Tanzania kwa kuzingatia mipango ya maendeleo.
“nimewaeleza wenzetu wa Italia kwamba maeneo ambayo wameyatambua yanaendana vizuri sana na agenda zetu” alisema Prof. Mkumbo.
Aidha, pamoja na mambo mengine, mkutano huo umefikia makubalino ya kujikita kwenye maendeleo ya zao la Kahawa kwa lengo la kuongeza uzalishaji, thamani na kupanua soko la zao hilo hasa barani Ulaya.
Hatua ya kubainisha zao la Kahawa kuwa la kipaumbele, inatokana na ukweli kwamba pande zote mbili, Tanzaia na Italia zina maslahi ya pamoja kwenye zao hilo.
Wakati Tanzania ikitegemea Kahawa kuzalisha ajira na kujipatia fedha za kigeni kwa mauzo ya nje, Italia ni wasambazaji wakubwa wa zao hilo, na Kahawa ni sehemu ya utamaduni wao.
“Tumekubaliana na wenzetu wa Italia kwamba tukitoka hapa tukaandae miradi katika maeneo haya matatu, namna ya kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa, namna ya kupata soko nchini Italia na namna ya kuongeza thamani ili tusafirishe kahawa iliyoongezewa thamani” Alifafanua Prof. Kitila Mkumbo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo mwenye dhamana ya kuratibu na kusimamia masuala ya Uwekezaji na Mipango nchini, miradi itakayobuniwa inatarajiwa kuisaidia nchi kukuza uchumi, kuongeza ajira na mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi.
Akiogoza ujumbe wa Italia katika mazungumzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Mhe. Stefano Gatti amesema pamoja na kuwa ushirikiano utalenga kukuza zao la Kahawa, Mpango wa Mattei utazingatia sekta ya Uchumi wa Buluu kwa upande wa Zanzibar.
Mhe. Gatti alisisitiza kuwa utekelezaji wa Mpango huo wa Mattei utahusisha kutoa elimu ili kujenga uwezo kwa sekta zote za miradi itakayotekelezwa.
Tanzania itaungana na nchi za Ethiopia, Kenya na Uganda katika utekelezaji wa miradi ya kilimo kwa kushirikiana na Italia.
Tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ameahidi kuchukua hatua za haraka za kuunda timu ya wataalamu itakayoungana na timu ya Italia kubuni miradi ya utetekelezaji.
Itakumbukwa kuwa, Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia walikutana Januari 28 – 29, 2024, Roma, Italia, ambapo Waziri Mkuu wa Italia Mhe. Giorgia Meloni alitangaza Miongozo ya Mpango wa Mattei kwa ajili ya maendeleo ya bara la Afrika.
Bila shaka, utekelezaji wa miradi inayotokana na Mpango kama huu, ni kielelezo tosha cha hatua za makusudi za Mhe. Rais, Dkt. Samaia Suluhu Hassan, za kuimarisha diplomaisa ya kiuchumi ili kujenga uchumi imara unaokaribisha ushiriki wa wawekezaji wa nje na ndani kwa kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria nchini.