Na Mwandishi wetu, Hanang’
WAGANGA wafawidhi wa zahanati na vituo vya afya mkoani Manyara wametakiwa kusimamia ubora wa huduma za afya kwa mama wajawazito katika vituo vyao ili kuendelea kupunguza idadi ya vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi wa MomCare tangu uingie Wilayani Hanang’ mwaka 2019 ni pamoja na kupungua kwa idadi ya vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua kutoka nane hadi viwili kwa mwaka, mafanikio ambayo kaimu mganga mkuu anataka yasirudi nyuma.
Wito huo umetolewa Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Manyara, (RMO) Melubo Mark wakati wa hafla ya kuhitimishwa kwa mradi wa MomCare wa shirika la FarmAccess.
Mark amesema miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi huo ulioanza mwaka 2019 ni pamoja na kupungua kwa idadi ya vifo hivyo wayaendeleze ili yasijirudie tena.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ (DMO) Dkt Mohamed Kodi amesema wakati shirika hilo likianza mradi huo mwaka 2019 idadi ya vifo vya wanawake waliokuwa wanaojifungua ilikuwa watoto nane ila hivi sasa ni vifo viwili kwa mwaka.
Amesema mbali ya faida hiyo mradi huo pia umesaidia kutoa elimu na kufanikisha asilimia kubwa ya wanawake wajawazito kutojifungua nyumbani na kwenda kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitalini.
“Kupitia mradi huu tuliweza kuwafuatilia kwenye mfumo wamama waliokaribu kujifungua na kuhimiza waende hospitali na vifaa vya kujifungulia walipata kwa wakati pindi wakihitaji,” amesema Dkt Kodi.
Mmoja kati ya wanawake waliojifungua watoto kupitia mradi huo Pendael Gwaltu amesema PharmAccess imefanikisha wanawake wengi wajawazito kutojifungua nyumbani.
“Binafsi kupitia mradi huu nimeweza kunufaika kwa kupata vifaa vya kujifungulia na elimu ya uzazi kabla na baada ya kujifungua watoto,” amesema Gwaltu.
Mkurugenzi wa miradi bunifu wa PharmAccess, Zamaradi Mbega amesema mradi huo ulianza mwaka 2019 na kuhudumia wilaya za Hanang’ na Babatii ukiwa na mafanikio mengi.
Mbega ametoa wito kwa halmashauri hiyo kusimamia mambo yote mazuri yaliyoanzishwa na mradi huo ili yaweze kudumu na kuwa faida kwa jamii.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hanang’ Francis Namahungo amewataka waganga na wauguzi kusimamia ubora wa huduma ili vifo visijirudie
Namahungo amesema mradi huo uliomalizika wa PharmAccess umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii.
Amesema pamoja na kupunguza vifo kwa kina wanawake wajawazito, jamii imekuwa na uelewa mpana kwa kufuata huduma za afya kwenye maeneo rasmi.