Na Mwandishi Wetu Dodoma
Jamii imeshauriwa kutokutumia nguvu nyingi wakati wa kupiga mswaki ili kutoharibu tabaka la juu la meno ikiwa ni Pamoja na matumizi ya dawa zenye mchanganyiko wa madini ya floride ili kulinda afya ya kinywa.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Dkt. Bingwa wa kinywa na meno kutoka St. Camillus Hospital Samweli Seseja wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya afya ya kinywa na meno inayoadhimishwa Tarehe 14-20/03 kila mwaka.
Dkt. Seseja amesema ili kulinda afya ya kinywa pia amewataka wananchi kutokula zaidi ya vyakula au vinywaji vya aina tano vilivyoongezwa sukari hasa sukari ya viwandani ili kulinda meno na kinywa chake.
Ameongeza kuwa kwa mtu mzima inashauriwa apige mswaki walau mara mbili kwa siku, aepuke matumizi ya pombe Pamoja na matumizi ya tumbaku ili kuepuka kupata saratani ya kinywa pamoja na kumuona mtaalamu wa kinywa na meno walau mara moja kwa mwaka.
Katika hatua nyingine Dkt. Seseja amewataka wazazi au walezi kuhakikisha pindi mtoto akianza kuota meno ndipo utaratibu wa kumsafisha uanze ili kuleta ustawi mzuri wa afya ya kinywa na meno kwa mtoto.
Maadhimisho ya afya ya kinywa na meno kwa mwaka huu yanafanyika Mkoni Pwani katika makao makuu ya wilaya kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha yakibeba na kauli mbiu isemayo “Kinywa chenye furaha, ni mwili wenye furaha”.