Na Khadija Khamis – Maelezo .
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma amewataka Wakuu wa Wilaya na Kamati zote za Maafa kutoa tahadhari za mapema kwa wananchi kuhama katika maeneo hatarishi ili kuepukana na maafa wakati wa mvua za masika .
Hayo ameyasema katika Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Vuga Zanzibar, wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Wenyeviti wa Kamati za Maafa za Wilaya na Kamati za Wataalamu wakati wa kujadili muelekeo wa Mvua za Masika ilioanza mapema wiki ya mwisho wa mwezi wa Febuari.
Amewapongeza na kuwapa moyo Wakuu wa Wilaya kwa kazi wanazozitekeleza na kuwataka kuendelea kuwapa elimu wananchi wanaoishi mabondeni na katika njia za maji ili kuhama mapema kabla ya athari kutokezea .
Amewashauri wenyekiti hao kushirikiana na masheha katika suala zima la usafi wa mitaro hasa ile inayopitisha maji ya mvua ili kujiweka tayari kwa mvua hizo zinazoendelea kunyesha.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Hamida Mussa Khamis amewaomba wananchi kupokea maelekezo ya kuhama mapema katika maeneo ya mabondeni ambayo huwaletea athari ya kupoteza Maisha na mali zao na kutafuta maeneo yaliyosalama.
“Naendelea kuwaomba wananchi kukubali kuhama katika maeneo hatarishi na kufuata maelekezo kwa sababu wao ndio wanaopata athari ” amesema Bi Hamida.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Makame Khatibu Makame amefahamisha kuwa kikao hicho ni cha kupata taarifa za muelekeo ya mvua ya masika ili kujiandaa kwa kupunguza athari katika maeneo hatarishi.
Amesema sula la maafa ni suala mtambuka hivyo kila mmoja asimame katika nafasi yake ili kutekeleza majukumu ya kusimamia utekelezaji wa kupunguza athari zinazosababisha maafa .
Mapema Mtaalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kanda ya Zanzibar Hassan Khatib Ame akiwasilisha mada ya muelekeo ya mvua za masika ya mwaka 2024 katika Visiwa vya Unguja na Pemba amesema kutakuwa na mvua ya wastani hadi juu ya wastani na athari mbali mbali zinaweza kujitokeza na kusababisha madhara .
Baadhi ya Wajumbe waliohudhuria katika Mkutano wa kujadili muelekeo wa Mvua za Masika kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Vuga Zanzibar.
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis akichangia Hoja katika Mkutano wa kujadili muelekeo wa Mvua za Masika kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Vuga Zanzibar.
Mtaalamu wa Hali ya Hewa Hassan Khatib Ame akiwasilisha mada katika hafla ya Mkutano wa kujadili muelekeo wa Mvua za Masika kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Vuga Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Makame Khatibu Makame akichangia hoja katika Mkutano wa kujadili muelekeo wa Mvua za Masika kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Vuga Zanzibar.