Waziri wa Nchi, Ofisi ya Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa wasimamizi wa kiwanda cha Lodhia, alipotembelea kiwanda hicho kilichopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
………
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amewataka wazabuni wanaopata tenda za Serikali kwenye eneo la ujenzi kutumia vifaa vinavyozalishwa ndani ya nchi ili kuokoa fedha za kigeni. Prof. Mkumbo ametoa wito huo leo, Machi 14, Mkuranga, Pwani alipofanya ziara ya kujionea maendeleo ya wawekezaji wazawa wa viwanda vya kuzalisha Nondo, Misumari, kofia za misumari na Mabati ambao ni kampuni ya Viwanda ya Lodhia. “Nimekuja kuona kama yale mambo tunayoyaona kwenye karatasi kwamba tumesajili miradi, ikiwa ni kweli tunayoyaona kwenye karatasi na kutoa taarifa yapo! nimefurahi kuona kwamba uwekezaji ni mkubwa, umezalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 600” Alisema, Prof. Mkumbo. Prof. Kitila alisema pamoja na kujihakikishia ikiwa uwekezaji wa kiwanda cha kuzalisha bati kichosajiliwa ni halisi, alifurahishwa na juhudi za mwekezaji huyo za kupanua viwanda vyake hasa cha kuzalisha nondo kwa kuongeza uzalishaji na ajira hadi kufikia 2000 tofauti na miaka miwili nyuma. “Nimesikiliza pia kero za mwekezaji, na jukumu letu ni kuangalia namna ya kutatua vikwazo wanavyokutana navyo wawekezaji tuboreshe mazingira yao, waendelee kufanya uwekezaji wazalishe ajira kulipa kodi tujenge uchumi wa nchi yetu”, alisema Prof. Mkumbo. Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Khadija Nassir, alisema kuwa Wilaya yake ina viwanda zaidi ya 100, na vingi vimejengwa ndani ya kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati huo huo, mmoja wa wamiliki wa viwanda vya Lodhia Bw. Sailesh Pandit, ameishukuru Serikali kwa kuwapa ushirikiano kila wanapohitaji. Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imekuwa mstari wa mbele kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini, hatua hizo zimechochea ongezeko la wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof.Kitila Mkumbo (katikati), Na Bi. Khadija Nassir, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga wakipokea maelezo kutoka kwa Bw. Sailesh Pundit mmoja wa wasimamizi wa kiwanda cha Lodhia, alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa wasimamizi wa kiwanda cha Lodhia, alipotembelea kiwanda hicho kilichopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani.