Umoja wa Wataalamu wa Afya wa Watanzania wanaoishi Uingereza (Tanzania-UK Healthcare Diaspora Association-TUHEDA} umetoa msaada wa Sanamu (Manikin) na vitabu, wenye thamani ya Shilingi milioni 130 kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani iliyopo Tumbi, Kibaha. Msaada huo ulikabidhiwa leo hosptalini hapo na Daktari bingwa wa magonjwa ya sukari, Bw. Nasibu Mwande na kupokelewa na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Tiba katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Caroline Damian.
Wakati akikabidhi msaada huo, Bw. Mwande alieleza kuwa sanamu hiyo ambayo imepewa jina la Msafiri inatumika kama mgonjwa wa kawaida kwa ajili ya kujifunzia na kuwafanya madaktari kuwa mahiri katika maeneo yao. Hatua hiyo inapunguza uwezekano wa madaktari kufanya makosa wakati wakiwa katika shughuli zao za kutibu wagonjwa. “Hii sanamu ni ya kisasa kabisa, kwa kutumia program maalum za computer unaweza kuifanya kuwa ni mgonjwa wa magonjwa mbalimbali kama ammonia, asthma au moyo kulingana na aina ya ugonjwa ambao watalaamu wa afya wamepanga kujifunza siku hiyo”, Bw. Mwande alisema.
Bw. Mwande alieleza zaidi kuwa sanamu za aina hiyo, zimewasaida Uingereza na Marekani kuwafanya wataalamu wao wa afya kuwa mahiri na kufanya kazi kwa pamoja (teamwork), kwani wakati wa kufanya mafunzo ya vitendo (simulation) kada zote za wataalamu zinazohitajika zinakuwepo.
Kwa upande wake, Dkt. Damian alipongeza TUHEDA kwa kuichagua na kuifanya hospitali ya Tumbi kuwa ya kwanza kupokea msaada huo kutoka kwao. Alisema hospitali ya Tumbi tokea zamani imekuwa kitovu cha elimu na kutokana na geografia yake, imekuwa ikihudumia majeruhi wa ajali za barabarani, hivyo uwepo wa sanamu hiyo ni msaada mkubwa kwa wataalamu wa afya na watu mbalimbali wataendelea kumiminika Tumbi kwa ajili ya kujifunza.
Makabidhiano hayo yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Diaspora kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Anisa Mbega. Katika hotuba yake, Balozi Mbega alisema kuwa msaada huo ni matunda ya Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Ubalozi wake wa Uingereza wa kuhamasisha Watanzania wanaoishi ughaibuni kuchangia uchumi wa nchi, na kwamba Wizara itaendeleza jitihada hizo ili kuunga mkono azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Balozi Mbega alieleza kuwa TUHEDA imejipanga kufanya mambo mengi kwa Tanzania na ili mambo hayo yaweze kutekelezwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakamilisha taratibu ili pande mbili hizo ziweze kusaini Hati ya Makubaliano (MoU).