Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Elimu Mhe.Deogratius Ndejembi,akizungumza wakati akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI cha kupitisha bajeti na mpango kazi kwa mwaka 2024/25 lililofanyika leo Machi 12,2024 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi na Naibu Katibu mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde ,akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI cha kupitisha bajeti na mpango kazi kwa mwaka 2024/25 lililofanyika leo Machi 12,2024 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Elimu Mhe.Deogratius Ndejembi,amelipongeza Baraza la wafanyakazi Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24.
Mhe.Ndejembi ameyasema hayo leo Machi 12,2024 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI cha kupitisha bajeti na mpango kazi kwa mwaka 2024/25.
Aidha Ndejembi amesema ili kuwepo na matokeo bora ya kiutendaji kazi katika kutoa huduma bora kwa wananchi lazima tija na maslahi viwe na uwiano.
“Hivyo ieleweke kuwa utendaji bora wa kazi na wenye tija kwa kuzingatia weledi na uwajibikaji utaiwezesha Serikali kuongeza mapato na hivyo kuwezesha kuongeza vile vile utoaji wa maslahi bora,”amesema.
Amesema kuwa madhumuni ya baraza la wafanyakazi ni kutoa fursa kwa watumishi kupitia kwa wawakilishi wao kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na maslahi yao kama watumishi kwa upande mwingine.
“Baraza la wafanyakazi linaongeza ushiriki wa wafanyakazi katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za taasisi kama ilivyo fafanuliwa katika sheria ya majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma sura namba 105,”amesema.
Aidha amewasisitiza kuwa mikutano ya mabaraza ya wafanyakazi itumike katika kujadili malengo na mipango ya taasisi ikiwa ni pamoja na maslahi ya watumishi na kuongeza kuwa mabaraza hayo yanatakiwa kujadili utendaji kazi wa kila siku na jinsi ya kuboresha utendaji kazi zaidi.
“Hapa nisisitize sana kuna umuhimu wa kila mtumishi katika kila taasisi kufahamu malengo ya taasisi ( Vision and Mission) ili tuweze kwenda pamoja na tusihiahi kama headless chicken kuku ukimkata kichwa anaruka ruka hujui Mission na Vision inakwenda wapi kwahiyo ni muhimu sana kujadili hayo katika mabaraza haya,”amesisitiza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi na Naibu Katibu mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde amesema baraza la wafanyakazi liliundwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2003 kama yanavyoundwa mabaraza mengine katika uwajibikaji na ndiyo linalounganisha kati ya wafanyakazi na wakuu wa idara wengine na kuwafanya kutimiza wajibu wao katika utendaji wa kazi.
Amesema moja kati ya ajenda zitakazojadiliwa katika kikao cha baraza hilo ni kuhusiana na bajeti itakayoenda kusomwa bungeni mwezi ujao pamoja na kupanga mpango kazi utakao wasaidia kufikia malengo yao.