Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Loiborsoit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Siria Baraka Kiduya amesema mpango wa bajeti uliopitishwa na Halmashauri hiyo utainufaisha Kata yake kupitia miradi mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kata yake juzi, Kiduya amesema wananchi wa vijiji vyake viwili vya Loiborsoit na Ngage, vitanufaika kupitia miradi ya maendeleo.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyofanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta ya elimu, afya, maji na mengineyo
Amesema kupitia bajeti ya halmashauri ya wilaya ya Simanjiro ya mwaka wa fedha wa 2024/2025, kata yake ya Loiborsoit imeweza kunufaika kupitia miradi tofauti ya maendeleo.
“Katika mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha wa 2024/2025 nimeweza kupata madarasa mawili ya shule shikizi ya Songoyo, sekondari ya Loiborsoit tumepata mradi wa UVIKO na pochi ya mama,” amesema Diwani huyo.
Amesema kwa upande wa sekta ya afya, anaishukuru serikali kwa kuhakikisha zahanati zote mbili zilizopo kwenye kata hiyo pia zinapatiwa miradi ili ziweze kuendelea kutoa huduma kwa jamii.
“Pia ninatoa pongezi kwa TARURA kwani daraja linalounganisha Wilaya ya Simanjiro na Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, lililopo kwenye kata yangu nalo limetengewa bajeti ya kujengwa,” amesema Diwani Kiduya.
Amesema mradi mkubwa wa maji wa mto Pangani nao umewanufaisha wananchi wa kata yake kwani shilingi bilioni 42 zimetengwa kwa kunufaisha Ngage na Loiborsoit, Ngarash na maeneo ya taasisi.
Amesema anatoa shukurani zake za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyotoa huduma kwa jamii hasa vijijini.
“Mwisho kabisa nawashukuru na kuwapongeza DC Simanjiro Dkt Suleiman Serera, Mbunge wa Jimbo Christopher Ole Sendeka, Mwenyekiti wa Halmashauri, Baraka Kanunga na Mkurugenzi Gracian Makota, kwa namna wanavyoongoza wilaya yetu ya Simanjiro,” amesema Kiduya.