Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa kituo cha polisi Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Mrakibu wa polisi (SP) Dominick Fwaja, amepanga askari watano kila kitongoji cha mji mdogo wa Mirerani, ili kupunguza uhalifu na kuhakikisha dhana ya polisi jamii na ulinzi shirikishi inapatiwa ufumbuzi.
SP Fwaja ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Serera wa kutembelea kitongoji kwa kitongoji na kusikiliza kero na changamoto za jami katika kata ya Endiamtu.
Amesema kwenye vitongoji vyote 24 vya mji mdogo wa Mirerani amewapanga askari polisi wanne au watano kwa kila kitongoji ili waweze kufanya kazi ya kulinda raia na mali zao kwa ukaribu zaidi.
Amesema ili kuhakikisha changamoto ya wizi, matukio ya uhalifu na vurugu zinamalizika, tumekaa kikao na wenyeviti wa vitongoji na kuwapatia askari polisi hao ambao watakuwa wanausika na vitongoji hivyo.
“Polisi wote wameshakutana na wenyeviti wa vitongoji na kutoa namba zao za simu hivyo wakiwa wanawahitaji wanawasiliana nao mara moja ili kukomesha matukio ya uhalifu,” amesema OCS Fwaja.
Mkuu huyo wa kituo amesema lengo ni kuhakikisha askari polisi hao wanashirikiana na wenyeviti wa vitongoji na wakazi wa maeneo husika katika kukomesha matukio ya uhalifu.
“Kwa ushiriano wao watamaliza mambo yote madogo yaliyopo kwenye uwezo wao na yale makubwa yatakayowazidi watayaleta kituoni tushughulike nayo,” amesema OCS Fwaja.
Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo, amempongeza OCS Fwaja kwa kutekeleza majukumu hayo ya kuwapangia askari polisi hadi ngazi ya vitongoji.
“Kupitia askari polisi hao waliopangwa kwenye vitongoji, ninatarajia wenyeviti na wakazi wa maeneo husika watawapa ushirikiano wa kutosha katika kupiga vita uhalifu,” amesema Kobelo.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Tanesko, Justin Abraham amesema hatua hiyo ni nzuri kwani hivi sasa uhalifu umepungua kwenye eneo lake kutokana na askari hao.
“Wezi wanaokuja kuiba hapa mtaani kwetu Tanesko siyo wakazi husika wa huku wanatoka maeneo mengine kuiba hata kuku, hivyo kupitia askari hawa na kamati yangu ya usalama tumekomesha wezi,” amesema.