Mtaalam wa mashine ya CT-Scan, Dkt. Charles Nchimbi akiwaelezea
wageni jinsi mashine hiyo inavyofanya kazi.
Dkt. Frida Shao kutoka Kitengo cha Magonjwa ya Dharura katika hospitali
ya Mloganzila (EMD) akiwaelezea wageni hao kazi zinazofanywa na
kitengo hicho.
Baadhi ya wabunge waliofika hospitali ya Mloganzila wakisikiliza mambo
mbalimbali yaliyokuwa yakizungumzwa katika kikao hicho.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-
Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi (kushoto), kulia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Afya ya Bunge la Korea ya Kusini, Bw. Kim Se-Youn
wakisikiliza utambulisho wa wageni waliofika hospitalini hapa.
Dkt Magandi katika picha ya pamoja na wabunge walioongozana na
mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Bunge la Korea ya Kusini waliokuja
kutembelea hospitalini hapa.
***********************************
Wabunge wa Serikali ya Korea ya Kusini wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati
ya afya ya Bunge hilo, leo wametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-
Mloganzila ili kufahamu huduma zinazotolewa hospitalini hapa.
Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wageni hao, Kaimu Naibu Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi
amewaeleza kuwa hospitali ya Mloganzila ina vifaa tiba vya kisasa na inatoa
huduma mbalimbali za afya ambapo kwa siku inahudumia wagonjwa wa nje 400
hadi 450.
“Hospitali yetu ina vifaa vya kisasa kama vile CT-Scan na MRI pamoja na kutoa
huduma kwa wagonjwa ambapo kwa siku tunawahudumia wagonjwa 400 hadi
450,” Amesema Dkt. Magandi.
Aidha Dkt. Magandi amefafanua kuwa lengo la kuanzishwa kwa hospitali kama ya Mloganzila ni ili kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi na badala yake kuimarisha huduma za afya zinazotolewa na wataalam nchini ili kuweza kutibu magonjwa ambayo hapo mwanzo yalihitaji mgonjwa kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Bunge la Korea ya Kusini,
Bw. Kim Se-Youn amesema kuwa wamefurahishwa na namna hospitali
inavyohakikisha kuwa jamii inayowazunguka inapata huduma bora za afya.
“Tumefurahi sana kuitembelea hospitali hii na tunatumaini kuwa hospitali ya
Mloganzila itaendelea kushirikiana na Serikali yetu ya Korea katika kuhakikisha
huduma bora za afya zinatolewa kwa watanzania,” Amesema Bw. Kim.
Wageni hao wametembelea kitengo cha magonjwa ya dharura (EMD), radiolojia
pamoja na maabara na kujionea namna wataalam wanavyofanya kazi.