Hakimu wa Wilaya ya Tabora Seraphina Nsana (kulia) akiwaapisha leo Viongozi wa Serikali wa Manispaa ya Tabora waliochaguliwa katika Uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita.
Baadhi ya Viongozi wa Serikali za Mitaa wa Manispaa ya Tabora wakiwa ya ukumbi wa Manispaa ya Tabora leo wakisubiri kuapisha na Hakimu wa Wilaya ya Tabora.
****************************************
NA TIGANYA VINCENT, TABORA.
VIONGOZI wa Serikali za mitaa waliochaguliwa wametakiwa kuwahudumia wananchi bila ya ubaguzi na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani ndiyo chanzo cha migogoro.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Tawala Wilaya ya Tabora Hammarskjold Yonaza wakati wa zoezi la kuwahapisha viongozi hao wa mita lilifanyika kwenye ofisi za Manispaa hiyo.
Yonaza alisema kuwa viongozi wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa wakitoa haki bila ubaguzi itasaidia kutimiza ndoto za wananchi waliowachagua za kuwaletea maendeleo na wao kuishi bila migogoro.
Alisema viongozi waliochaguliwa ni vema wakatanguliza maslahi ya waliowachagua na kutimiza matarajio yao ili wazidi kupata maendeleo.
Alisema kama wasipotenda haki ina maana watakuwa wameshindwa kuongoza na kutoa fursa ya kuwepo migogoro kwenye maeneo yao jambo ambalo halikubaliki.
Aidha Katibu Tawala huyo aliwaonya kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinasababisha kuzalisha migogoro katika jamii na kuwatia aibu wao wenyewe pindi watakapobainika.
Kwa upande wa Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Manisapaa ya Tabora William Mpangala alisema kuwa Manispaa hiyo yenye Mitaa 134, wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) 126 walipita bila kupingwa na Mitaa nane ndio iliyofanya uchaguzi pia wagombea wa Chama hicho wameshinda.
Aliongeza kuwa Chama cha Mapinduzi pia kilinyakuwa Viti vyote vya wenyeviti wa vitongoji 41 na vijiji 156 baada ya wagombea wake kupita bila kupingwa.
Mpangala alisema alisema walitoa elimu hiyo kwa viongozi wa ngazi ya wilaya wa Vyama vyote juu ya ujazaji fomu lakini bahati mbaya inaelekea hawakuifikisha kwa wanachama wao ngazi za chini wakiwemo wagombea jambo lilipelekea majina yao kuengeliwa.
Alisema kuwa matokeo ya kutoipeleka elimu hiyo kwa wanachama wao,wengi walishindwa kujaza famu na hivyo kuonekana walishindwa kwa kukosea kuzijaza inavyotakiwa.
Mpangala alivitaka siku za baadaye ,vyama vya Siasa kuhakikisha vinatoa elimu ya uchaguzi kwa wanachama wao wa ngazi za chini ili jambo kama hilo lisitokee katika chaguzi zijazo.
Viongozi hao waliapishwa na Hakimu wa Wilaya ya Tabora,Seraphina Nsana,katika Ofisi za Manispaa ya Tabora.