Bi. Lenes Masebo Mkazi wa Itumba wilayani Ileje mkoani Songwe atembelewa na Mtandao wa Polisi wanawake Mkoa wa Songwe kwa ajili ya kumpa msaada wa vitu mbalimbali kwa matumizi ya nyumbani.
Msaada huo umekuja kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani baada ya Polisi kata wa kata hiyo Koplo Yasinta kugundua bibi huyo anaishi kwenye mazingira magumu na anauhitaji wa kusaidiwa kutokana na bibi huyo kuishi na wajuuku wake wanne bila kuwa na msaada wa mtu yeyote baada ya kufiwa na watoto wake 08 kati ya 10 aliowaza ikiwa pamoja na mume wake na kubakiwa na watoto 02 ambao nao hawana uwezo wa kumsaidia na wanaishi nje ya Mkoa wa Songwe.
Akizungumza baada ya kukabidhi mahita hayo Machi 06, 2024 Mkuu wa Kituo cha Polisi Vwawa, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Veronica Myovela kwa niaba ya askari waliomtembelea bibi huyo amesema kuwa ni muhimu kutoa kwa watu wanaoishi kwenye mazingira magumu na wenye uhitaji ili kuwatia moyo na kuwaleta karibu na jamii.
Naye, Bi. Lenes amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kumtembelea nyumbani kwake na kumpa mahitaji hayo, “nimefurahi kwa kitendo cha Jeshi la Polisi kunitembelea na kunipa msaada wa vitu mbalimbali, namshukuru Mungu kwa kuwaongoza Askari hawa, nawaombea kwa Mungu aibariki kazi yao” alisema Bi Lenes.