TAASISI ya Agape Mission Tanzania imempongeza Rais John Magufuli kwa kupitisha uamuzi wa kuwepo elimu bure hadi kidato cha nne kwani wanafunzi wengi hasa wa wazazi na walezi wenye kipato duni wametumia fursa hiyo kupiga hatua kielimu.
Mkurugenzi wa Agape Mission Tanzania, Mchungaji Canon, Kedmon Mlemeta aliyasema hayo kwenye mahafali ya tano ya shule ya sekondari Mgutwa ya wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Mchungaji Canon Mlemeta alisema dhana ya elimu bure ya Rais Magufuli ina manufaa makubwa mno kwa jamii kwani Taifa litakuwa na wasomi wazuri na nchi itainuka kupitia taaluma mbalimbali.
“Wengine watakuwa maprofesa, madaktari, walimu, wahandisi, wataalamu wa mifugo, kilimo, ujenzi, uashi na taaluma mbalimbali, hiyo yote ni kupitia dhana ya elimu bure ya Rais Magufuli,” alisema.
Aliwapongeza watumishi, walimu na wanafunzi wa shule ya Mgutwa kwani ilipoanzishwa wengine walibeza na kuicheka kuwa ipo porini lakini sasa imepiga hatua.
“Napata simu nyingi kutoka kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne hapa Mgutwa, wengine wapo vyuo mbalimbali ikiwemo IFM, UDOM, wengine wamesomea ualimu wanataka kuja kufanya mazoezi hapa, hayo ndiyo mambo tunayotaka,” alisema.
Mgeni rasmi wa mahafali hayo, ofisa Tarafa ya Moipo, Joseph Mtataiko aliipongeza shule ya Mgutwa kwa kutunza mazingira kutokana na kugawa miche kwenye taasisi mbalimbali.
“Mmegawa miche kwenye shule na taasisi mbalimbali pia kule katika uwanja wa wazi wa soko na mnada wa Songambele kata ya Mirerani miti mingi mliipanda na sasa imekuwa mikubwa,” alisema Mtataiko.
Mkurugenzi wa shule ya sekondari Mgutwa, Shedrack Mlemeta alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2012 kwenye kata ya Shambarai mpakani na mji mdogo wa Mirerani.
Mlemeta alisema shule hiyo ya sekondari Mgutwa imepiga hatua kwani imeanzisha kidato cha tano kuanzia mwakani itaanza kupokea wanafunzi wa hatua hiyo.
Alisema wametoa upendeleo kwa wanafunzi 23 waliohitimu kidato cha nne kusoma kozi ya kompyuta itakayoanza Januari mwakani.
“Pia tumeanzisha kituo cha kufanyia mtihani wa kidato cha nne QT hivyo wale wote wenye kuhitaji huduma hiyo mnakaribishwa sana mjiandikishe hapa Mgutwa,” alisema.
Mmoja kati ya wahitimu wa mahafali hayo, Mary Mndolwa akisoma risala alisema walianza kidato cha kwanza mwaka 2016 wakiwa wanafunzi 48 ila wamehitimu wanafunzi 23 pekee.
Mndolwa alisema wanafunzi wote wanawashukuru walimu na uongozi wa shule hiyo kwa kuwasimamia kitaaluma na nidhamu, kwa kuwalea kimwili na kiroho.
Katika mahafali hayo iliendeshwa harambee ya ghafla ya umaliziaji wa jengo la maabara ya wanafunzi wa shule hiyo na kupatikana sh600,000.