Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy
Gwajima akiwa katika picha ya Pamoja na watoto wa kituo cha matumaini
kilichopo Miuji Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy
Gwajima akifurahia kumbeba mtoto Queen wakati alipotembelea kituo cha
kwatoto cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy
Gwajima akizungumza na mtoto wakati akikagua kituo wakati wa ziara yake
katika kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy
Gwajima akifurahi katika picha ya Pamoja na mtoto Maria wa kituo cha
matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma.
Afisa Ustawi wa Jamii toka OR-TAMISEMI anayeshughulikia watoto
wanaoishi katika mazingira hatarishi Nkinda Ziada Shekalaghe akizungumza
wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu Dr.Dorothy Gwajima.
Baadhi ya watoto katika picha ya pamoja wakimskiliza Dr.Dorothy Gwajima
wakati wa ziara yake katika kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini
Dodoma.
**********************************
Atley Kuni, OR- TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Doroth Gwajima
amewataka wazazi na walezi kuwa makini na kuimarisha ulinzi na usalama wa
mtoto wakati wa msimu sikukuu ya Eid.
Dr.Gwajima ameyasema hayo alipotembelea kituo cha kulelea watoto cha
Nyumba ya matumaini kilichopo Kata ya Miuji Jijini Dodoma na kutoa misaada ya
vitu mbali mbali kwa ajili ya sikukuu.
“Ni wajibu wa kila mzazi kutekeleza jukumu lake la msingi la kuhakikisha mtoto
yuko salama na anasherekea sikukuku katika mazingira rafiki na yenye kumjenga
kimwili na kiakili zaidi bila kupata dhahama ya aina yeyote” Alisema Gwajima.
Aidha Dr. Gwajima amekipongeza kituo hicho kwa jukumu kubwa walilo nalo
lakuhakikisha watoto waliopo hapo wanapata malezi bora huku akiwaasa watoto
kuzidisha upendo na mshikamano miongozi mwao.
“Tunatekeleza hili kwakuwa ni wajibu wetu kuwalea watoto kwani hata sisi leo
tumekuwa watu wazima kwa sababu ya juhudi za wakubwa zetu, nanyi watoto
mtakuwa wakubwa kama sisi na mtakuja kuwa viongozi wa taifa hili katika nyanja
mbali mbali, hivyo pendaneni na kuishi kwa amani na msome kwa bidii” alisema
Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya ustawi wa
Jamii, OR-TAMISEMI, Rashed Maftah, alisema zoezi hilo ni moja ya majukumu yao
ya msingi na wajibu wao katika kuzihudumia Mamlaka zote 184 nchini katika
kuhakikisha watoto waliokatika mazingira magumu wanapata vituo vya kuwalea
katika misingi bora na usalama wao unaimarika.
“Dini iliyosafi ni yenye kuwajali Yatima na wenye uhitaji kwa kuunganika na
kushiriki nao katika mahitaji yao ya Msingi, aidha Sheria ya mtoto namba 21 ya
mwaka 2009 kanuni ya 12 inahimiza suala la kulelea watoto” Alisema Maftah.
Akizungumza kwa niaba ya Walezi wa kituo hicho, mmoja ya walezi, Sister Urea,
alisema kituo hicho kina jumla ya watoto 63 na kimekuwa kikifanya kazi zake toka
mwaka 1995 kwa kuhudumia watoto wanaopatikana katika mazingira magumu na
ukatili wa kijinsia kutoka mikoa ya Dodoma na Singida.
Akishukuru kwa niaba ya wenzake mtoto Mariah Zahoro, alimshukuu Naibu
Katibu Mkuu na ujumbe wake huku akiomba zoezi hili lisiwe la mwisho bali liwe
endelevu kwani wanapopata wageni wanao watembelea wanafarijika sana.
“Tunawashukuru sana kuja kutuona na kutupatia misaada, lakini msiishie kuja
kuleta misaada tu, hata kama hamna kitu msisite kuja kutusalimia na kuongea na
sisi, tunaomba Mungu awazidishie pale mlipotoa na siku nyingine tena
mtukumbuke” alisema Mariah.
Kwa Mujibu wa Afisa Ustawi wa Jamii kutoka jijini Dodoma, kituo cha Nyumba ya
Matumaini kilichopo Kata ya Mihuji ni moja kati ya vituo vinane vilivyopo ndani ya
Halmashauri hiyo ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kulinda haki za watoto.