Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mapema leo, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse ,Ikulu jijini Dodoma.
Bw. Tadesse akiwa ameambatana na ujumbe wake amewasili uwanja wa ndege wa jijini Dodoma leo, Novemba 25, 2019 na kulakiwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango, na Mkuu wa Itifaki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge.
Akizungumza muda mfupi baada kumaliza mazungumzo na Mheshimiwa Rais Magufuli, Bw. Tadesse amesema TDB itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania na kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali maendeleo nchini.
Mhe. Dkt. Mpango amesema TDB imekuwa moja ya Benki kinara ambayo imekuwa ikitoa mikopo ya masharti nafuu kwa Tanzania hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye miradi ya maendeleo.
Aidha, Bw. Tadesse akiwa nchini atatembelea maeneo mbalimbali sambamba na kujionea miradi ya maendeleo inayotelezwa na Serikali ikiwemo miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, mradi wa kuzalisha umeme wa Kilwa na miradi mingine ambayo mkopo kutoka (TDB) utaelekezwa.
Bw. Tadesse amesifu jitihada zinazofanywa na Serikali katika kufanya mageuzi ya kiuchumi nchini na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Viongozi na Watendaji wa Serikali wakiwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse mara baada ya kumlaki katika uwanja wa ndege jijini Dodoma. |