Katika juhudi za kukuza ubora wa elimu na kuhakikisha watoto wa kike wa vijijini wanapata elimu bora, shirika la Lyra in Africa limezindua bweni la wasichana na chumba cha kompyuta vyenye thamani ya jumla ya zaidi ya shilingi milioni 845 katika shule ya Kata ya Mseke, mkoani Iringa.
Shirika hilo lisilo la kiserikali ambalo limejikita katika kuboresha mazingira ya shule za sekondari za umma kwa lengo la kukuza ubora wa elimu limesema kwamba zaidi ya kujenga miundombinu na kugawa vifaa vya tehama vitakavyosaidia wanafunzi na walimu katika shule hiyo, inalenga pia kuwalinda wasichana kutokana na hatari mbalimbali zinazotokana na kutembea umbali mrefu pamoja na hali ngumu ya maisha kwa ujumla.
Katika uzinduzi uliofanyika Februari 20 ambapo Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Veronica Kessy alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Lyra kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Bi. Cikay Richards ilitanabaisha dhamira thabiti ya shirika hilo kushirikiana na jamii pamoja na serikali katika kuchochea maendeleo ya elimu na uchumi.
“Dhamira yetu inakwenda mbali zaidi ya ujenzi wa miundombinu na kugawa vifaa vya tehama. Tumejitolea kukabiliana na changamoto za kimfumo zinazowakabili wasichana wadogo katika kupata elimu bora lakini zaidi kupambana na umaskini ambalo ndio chimbuko kuu la changamoto za elimu”, alisema Bi. Richards.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bi Veronica Kessy aliwapongeza Lyra in Afrika na washirika wake ambao ni Softcat, Greensafe na Michael Matthews Foundation kwa kusimamia na kufadhili mpango huo wenye manufaa makubwa kwa jamii kwa ujumla.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Lyra in Africa kwa kuratibu mradi huu sambamba na wafadhili na serikali kwa mchango wake,” alisema Bi. Kessy. Kujitolea kwao kunawawezesha wasichana na vijana wetu kupata elimu katika kiwango kinachokubalika,” aliongeza.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mseke, Ernest Sakafu alionyesha shukrani zake kwa Lyra kwa mchango mkubwa shuleni hapo.
“Lyra imekuwa chachu ya mabadiliko katika shule yetu,” alisema Bw. Sakafu. Ujenzi wa bweni na utoaji wa vifaa vya tehama utainua uwezo wa kielimu kwa wanafunzi wetu, haswa watoto wa kike ambao wamekuwa wanapata changamoto ya kutembea umbali mrefu.”, aliongeza.
Debora Damas Kasela, Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Mseke, aliunga mkono maoni hayo, akisisitiza mchango mkubwa wa Lyra katika maisha ya wanafunzi. “hatutapitia tena ugumu wa kulala kwenye sakafu ya darasa,” alisema Debora. “Lyra imetupa hadhi mpya ya utu wetu na imeamsha uwezo wetu wa kunufaika na elimu.”
Wakati Tanzania inapopiga hatua kuweka mazingira bora ya elimu na usawa wa kijinsia kwa kuweka mazingira wezeshi na matumizi ya tehama katika kufundisha na kujifunza, juhudi za Lyra ni mfano wa kuigwa katika kufikia malengo hayo.