MKURUGENZI Mtendaji wa Digitali Agenda For Tanzania Initiative Peter Mmbando,akitoa taarifa ya Matokeo ya ripoti zilizofanywa na Taasisi ya Digital Agenda Tanzania Initiative kuhusu utambuzi wa kutumia taarifa za Kibayometriki,wakati wa Kikao cha kujadiliana kuhusu utetezi wa haki kidigitali kilichofanyika leo Februari 23,2024 jijini Dodoma.
MCHAMBUZI wa Sera na Mtaalamu wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini Tanzania,Mrisho Swetu,akitoa elimu kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi wakati wa Kikao cha kujadiliana kuhusu utetezi wa haki kidigitali kilichofanyika leo Februari 23,2024 jijini Dodoma.
MKURUGENZI Mtendaji wa Digitali Agenda For Tanzania Initiative Peter Mmbando ,akiwa katika picha ya pamoja na washiriki mara baada ya Kikao cha kujadiliana kuhusu utetezi wa haki kidigitali kilichofanyika leo Februari 23,2024 jijini Dodoma.
Na. Gideon Gregory, Dodoma.
Wataalamu kutoka Taasis ya Digital Agenda for Tanzania Initiative imekutanaa pamoja na wadau kutoka Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari wamekutana leo Februari 23,2024 Jijini Dodoma kujadiliana kuhusu utetezi wa haki kidigitali.
Lengo la kikao hicho ni kutoa matokeo ya ripoti mbili zilizofanywa na Taasisi ya Digital Agenda Tanzania Initiative kuhusu utambuzi Kwa kutumia taarifa za kibayometriki,usajili wa laini za simu unaofanywa na Makampuni ya simu nchini.Tafiti imebainisha kuwa makampuni ya simu nchini licha ya kufanya vizuri katika kutoa huduma lakini bado kuna mapungufu katika kulinda haki ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi zonazowahusu wateja wao.
Akibainisha mapungufu hayo mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo Peter Mmbando amesema kuwa ulinzi wa data, uhuru wa kujieleza pamoja na uendeshaji wake vilibainika kuwa ni moja kati ya mapungufu ya mitandao hiyo.
Mmbando amesema kuwa, elimu zaidi Kwa wananchi inapaswa ku ndelea kutolewa ili kuhakikisha taarifa zao zinakuwa salama pamoja na kuhakikisha wanaepukana na makosa ya kimtandao ambayo yamekuwa yakifanyika.
Kwa upande wake Mtaalamu wa ulinzi wa taarifa binafsi Nchini Tanzania,Mrisho Swetu ameitaka jamii kuamka na kuwa mstari wa mbele katika kulinda taarifa zao. Amesisitiza kuwa taarifa binafsi nyeti za kibayometriki mfano alama za vidole zina Athari kubwa endapo zitatumika vibaya.
Pia ameendelea kuhimiza wadhibiti na wachakataji wa taarifa binafsi Nchini kuboresha viwango vya ulinzi wa taarifa binafsi pamoja na kuendelea kutoa elimu ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa mujibu wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi,2022. Wadhibiti na wachakataji wanapaswa kuheshimu haki ya faragha na hyo itasaidia kuongeza uaminifu na wateja wao.
Kwa upande wa Jamii amesema,wadau wa serikali na sekta binafsi waendelee kutoa elimu kwa umma kuhusu haki ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi.Jamii inapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi pamoja na haki zao kama haki ya kuomba kufutwa kwa taarifa zako,haki ya kurekebisha,haki ya kupata fidia pale itakapotokea misingi ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi imekiukwa.
Aidha,ameendelea kusema, mafunzo hayo wamelenga kuyafikia makundi yote katika jamii, mikoa yote ambapo kwa upande wa watu wenye ulemavu wa kuona na kusikia wapo kwenye mpango wa kukutana na wataalamu wa lugha ya alama ili kujua elimu hiyo itawafikiaje jamii hiyo ya watu wenye ulemavu.
“Lengo ni kuikumbusha jamii matumizi sahihi ya taarifa binafsi,kujua haki zao ,lakini ni muhimu wafahamu kuwa taarifa zao binafsi zikitumika vibaya zinaweza kuleta madhara,lakini wafahamu kuwa endapo kutatokea uvunjifu wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi basi ni wapi wanaweza kupeleka malalamiko yao” Amesema Mrisho Swetu
Naye, Afisa Mwandamizi Tume ya Haki za binadamu za Utawara Saidi Zuberi amesema mafunzo hayo yatakwenda kumasaidia mwananchi kuweza kulinda taarifa zake na kutambua haki za faragha.
Pia ametoa wito kwa watoa elimu wa tume ya ulinzi wa data kuwa na miongozo itayoweza kutoa elimu ya haki ya faragha katika jamii .