Miongoni mwa shamba la mahindi wilayani Namtumbo ambalo mmiliki wake amepata mkopo wa pembejeo kutoka Benki ya NMB wilayani humo.
Afisa mahusiano wa Benki ya Nmb tawi la Namtumbo mkoani Ruvuma Simon Mhaya akiangalia uzalishaji wa mahindi katika shamba la mkulima Fadhil Kitete ambaye amepata mkopo wa pembejeo kutoka Benki hiyo.
Mkulima wa mahindi Fadhil Kitete kulia,akimuonyesha Afisa mahusiano wa Benki ya Nmb tawi la Namtmbo Simon Mhaya moja kati ya shamba lake la mahindi ambalo ametumia pembejeo baada ya kuwezeshwa mkopo kutoka Benki ya Nmb.
Na Muhidin Amri,
Namtumbo
WAKULIMA wa zao la mahindi wilayani Namtumbo,wameishukuru Benki ya NMB kwa kutoa mikopo ya pembejeo za kilimo kwa wakati,hali itakayowezesha kuongeza uzalishaji wa mazao kwa msimu wa kilimo 2023/2024.
Walisema,misimu iliyopita walishindwa kufanya vizuri katika uzalishaji kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya maandalizi ikiwemo kununua mbolea na mbegu za bora, badala yake walipanda kwa kutumia mbegu za kizamani ambazo uzalishaji wake ni mdogo na wengine walilima bila kutumia mbolea.
Fadhil Kitete alisema,benki ya NMB imewatendea haki kutoa mikopo ya pembejeo kwa muda muafaka,hivyo wakulima ambao ni wateja wa benki hiyo wamefanikiwa kuandaa mashamba yao mapema na kuwahi msimu mpya wa kilimo.
Kitete,ameiomba serikali kupitia wizara ya kilimo kuhakikisha inawajali wakulima wadogo kwa kuwapatia mikopo ya riba nafuu ili waweze kuzalishaji kwa tija na kuondokana na umaskini kupitia shughuli zao za kilimo.
Aidha,ameiomba serikali kuwatafutia masoko ya uhakika ya mazao yao,badala ya kuwa mstari mbele kwa kuhimiza uzalishaji kila unapoanza msimu mpya wa kilimo na kuwaacha yatima pale inapofika msimu wa ununuzi wa mazao yao.
Ametoa wito kwa wananchi hasa wakulima,kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na NMB kwa riba nafuu ili waweze kunufaika na kuacha tabia ya uwoga ambayo imekuwa chanzo cha kuongezeka kwa umaskini kwa wananchi wengi katika wilaya hiyo.
Said Ngonyani mkulima wa zao la Tumbaku,ameiomba wizara ya kilimo kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kukopesha wakulima ili kuwavutia na kuwashawishi watu wengi kupenda kujihusisha na shughuli za kilimo.
Alisema, baadhi ya wananchi hasa vijana wanaona kilimo ni adhabu kutokana na changamoto nyingi wanazokutana nazo kama vile bei kubwa ya pembejeo na kukosa soko la uhakika la kuuzia mazao wanayozalisha.
Kwa upande wake Afisa mahusiano wa Benki ya NMB tawi la Namtumbo Simon Mhaya alisema,katika msimu wa kilimo 2023/2024 wametoa mikopo ya kilimo kwa vikundi 103 vyenye wanachama zaidi ya 2,000 wanaojihusisha na kilimo cha mazao ya mahindi,ufuta,mbaazi,mpunga na Tumbaku.
Pia alieleza kuwa, katika msimu wa mwaka 2022/2023 Benki ya NMB ilitoa mikopo kwa vikundi 51 vyenye watu zaidi ya 103 wanaojihusisha na shughuli za kilimo katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Kwa mujibu wa Mhaya,mikopo hiyo imesaidia kuleta maboresho makubwa ya kibenki na lengo ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,ya kupanua wigo wa kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
“benki yetu inatambua umuhimu wa kujitoa katika kuisaidia jamii,hivyo tutaendelea kutoa mikopo siyo kwa wakulima tu bali pia kwa watu wengine wanaohitaji fedha kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi”alisema Mhaya.
Mhaya,amewataka wateja wanaochukua mikopo kuhakikisha wanatumia fedha hizo kwa malengo na kurejesha kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza na benki iweze kukopesha watu wengine wenye uhitaji wa fedha.