Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
MWENYEKITI wa Baraza la Vyama Vya Siasa nchini, John Shibuda, amewataka Watanzania wajitokeze kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika kesho.
Pamoja na hali hiyo amesema kuwa ni wajibu wa kila mtanzania kuchaguzi kiongozi anayemtaka kwani hatua hiyo itasaidia kujenga misingi ya utawala bora katika upatikaji wa viongozi hao.
Hayo aliyasema jana kupitia taarifa ailiyoitoa kwa vyombo vya habari ambapo aliwataka watanzania kujitokeza na kwenda kupiga kura kuchaga viongozi hao pamoja na wajumbe wao.
“Natoa wito kwa umma wote mjitokeze na kwenda kupiga kura. Wito unazingatia kwamba kamati ya uongozi ya Baraza la vyama vya siasa Tayari imechukua hatua ya kusimamia kutendeka kwa hatua za kutakatisha hitilafu zote, zinazoathiri sifa za uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019.
“Kwa hiyo sasa, nashauri kila mtu mwenye sifa za kupiga kura na alikuwa amekwazika na kero za watendaji waitwao waborongaji wa kanuni za uchaguzi huu. Sasa nawashauri watu wote muwe na ufikiri mwema wa kuunda uamuzi mpya wa kushiriki katika uchaguzi huu wa kuchagua viongozi wa serikali za mitaa. Kwa hiyo jitokezeni mkapige kura siku ya Novemba 24, 2019 (kesho),” alisema Shibuda.
Aliwataka wananchi, wanasiasa na wakereketwa wa demokrasia na siasa za ushindani wa vyama vingi kutambua kwamba kususia upigaji kura sio ubani wa sadaka ya kafara la kuondoa matendo batili ya kuundika kwa mazalia ya hila za athari za kiini macho kwa haki na usawa za mfumo wa vyama vingi.
“Ukombozi dhidi ya tabia za matendo ya watekelezaji maovu ya hulka potofu, dawa yake ni vikao vya kukosoana Tupate masahihisho ya kujenga. Stahiki katika utungwaji wa kanuni mpya za uchaguzi.
“Kwa hiyo sasa, nawashauri wananchi, viongozi wa siasa na wakereketwa wa siasa kataeni kuwa mateka wa hasira za kuwapa ushindi waborongaji na waparaganishi wa kukwaza dhamiri zenu za kushiriki katika upigaji kura,” alisema
Shibuda ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa vyama vya CCM na Chadema kwa nyakati tofauti, alisema Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya siasa ndiyo sauti kuu, hivyo vikao hivi vitawaarifu kuhusu matokeo ya kikao cha majadiliano na wasimamizi wa uchaguzi huu wa serikali za mitaa.