Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola ,ambaye ataongoza Mkutano wa Tatu wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2023/2024 unaotarajiwa kuanza Jumatatu tarehe 19 Februari 2024, jijini Dodoma. |
Na Mwandishi Wetu , Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola anatarajiwa kuongoza Mkutano wa Tatu wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2023/2024 unatarajiwa kuanza Jumatatu tarehe 19 Februari 2024, jijini Dodoma.
Bw. John C. Mbisso Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma kupitia taarifa kwa vyombo vya habari aliyoitoa Jijini Dodoma leo tarehe 16 Februari 2024 amesema kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 [Marejeo ya mwaka 2019], Tume ya Utumishi wa Umma ina jukumu la kupokea na kushughulikia Rufaa za mashauri yaliyotolewa uamuzi na Mamlaka za Nidhamu.
“Tume katika kutekeleza jukumu hili itafanya Mkutano wake wa Tatu katika mwaka wa fedha 2023/2024 uliopangwa kufanyika kwa muda wa wiki Tatu Jijini Dodoma, kuanzia tarehe 19 Februari 2024 hadi tarehe 08 Machi 2024. Tume itapokea, itajadili na kutolea uamuzi Rufaa na Malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa na Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka zao za Nidhamu’ amesema Bw. Mbisso.
Kupitia taarifa hiyo amefafanua kuwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 62 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, wakati wa Mkutano kuna baadhi ya Warufani pamoja na Wawakilishi wao walioomba kufika mbele ya Tume kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao za rufaa walizowasilisha Tume.
Bw. Mbisso amehitimisha taarifa yake kwa kusema kuwa, shughuli nyingine zilizopangwa kufanyika wakati wa Mkutano ni kupitia taarifa mbalimbali za utendaji wa Tume.