Mkuu wa wilaya ya Igunga moani Tabora Sauda Mtondoo akiwa amemlea mtoto Betina Frank (3) akipatiwa chanjo ya Surua, Rubella na muuguzi aliye upande wa kushoto Monica Samila kwenye kiwanja cha hospitali ya Igunga wakati wa uzinduzi wa chanjo.
Mkuu wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora Sauda Mtondoo akiwasha gari mojawapo kati mawili ya kubebea wagonjwa wakati wa uzinduzi wa chanjo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassani
Mkuu wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora Sauda Mtondoo (kulia) akimkabidhi funguo za magari mawili ya kubebea wagonjwa yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassani mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Selwa Abdallah Hamid aliyeko kushoto wakati wa zoezi la uzinduzi wa chanjo ya surua, Rubella
Na Lucas Raphael,Tabora
Mkuu wa Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, Sauda Mtondoo azindua chanjo ya Surua na Rubella pamoja na kugawa magari mawili ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya hospital ya wilaya ya igunga mkoani Tabora
Magari hayo yametolewa na serikali huku akiwataka wananchi wilayani hapa kuwapuuza wale wote ambao wamekuwa wakipita mitaani na kuwapotosha wananchi kuhusu suala zima la chanjo.
Alitoa kauli hiyo jana katika uzinduzi wa zoezi la chanjo lililofanyika katika uwanja wa hospitali ya wilaya ya Igunga ambapo zaidi ya akina mama 400 walijitokeza kwenye zoezi hilo la kupatiwa chanjo watoto wao.
Mtondoo alisema kuwa lengo kuu ni kufanikiwa kuwachanja watoto kwa asilimia 100 ambapo imethibitika kuwa chanjo ni mkakati muafaka katika kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano na kupelekea kupunguza gharama kubwa kwa familia na taifa kwa ujumla.
“Halmashuri yetu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali wa maendeleo wamekuwa wakitoa chanjo kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano dhidi ya magonjwa mbalimbali kama vile kifua kikuu, dondakoo, kifaduro, homa ya ini, kuhara, vichomi, homa ya uti wa mgongo, kupooza, surua, rubella na pepopunda. Hii ni katika harakati za kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo,” Alisema Mtondoo.
Sambamba na kuzindua zoezi la chanjo, pia alikabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa kwa jimbo la Igunga mjini na Manonga ambayo yatatatua changamoto kwa wagonjwa wanaozidiwa na kuwahishwa Hospitalini, huku akimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kupitia Wizara ya Afya kwa msaada huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Selwa Abdallah Hamid akiwataka wale wote waliokabidhiwa magari hayo kuyatumia kwa kazi iliyokusudiwa na endapo yatatumika kinyume na lengo lililokusudiwa hatosita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga Dkt Lucia Kafumu, alibainisha kuwa chanjo huzuia takribani ya vifo milioni 3 kila mwaka kutokana na maradhi yanayokingwa kwa chanjo duniani.
Ambapo kwa nchini Tanzania mafanikio ya chanjo yameonekana dhahiri kwa mfano kufanikiwa kutokomeza ugonjwa wa ndui, kupunguza magonjwa ya kuhara na kichomi (Nimonia) ambayo yalikuwa yanaongoza kuwalaza watoto Hospitalini. Mafanikio haya makubwa yametokana na kuwapatia chanjo watoto kwa zaidi ya asilimia 90 walio chini ya umri wa mwaka mmoja.
“Pamoja na mafanikio haya makubwa bado tunayo changamoto ya watoto ambao hawajakamilisha ratiba ya chanjo kulingana na umri wao, watoto hawa wako kwenye hatari ya kupata milipuko ya magonjwa na kuhatarisha jamii nzima.
Alisema kwa mwaka 2022 hadi 2023 kulitokea mlipuko wa ugonjwa wa Surua nchini na mkoa wetu wa Tabora pamoja na wilaya yetu ya Igunga ilipata mlipuko wa Surua na watu wapatao 81 waliugua ugonjwa huo ambao ni zaidi ya asilimia 50 wakiwa watoto chini ya miaka mitano.”
Hata hivyo alifafanua kuwa lengo la kampeni hiyo kwa mwaka 2024 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga wamelenga kuwafikia watoto wapatao 96,983 ambao ni watoto wote walio na umri kuanzia miezi 9 hadi miaka mitano ambao wanatakiwa kufikiwa na kupatiwa chanjo ya Surua na Rubella huku akibainisha kuwa wamedhamiria kuvuka lengo hilo kwa zaidi ya asilimia 100 na kuwafikia watoto wote wilayani hapa.
Kwa upande wa kinamama waliopeleka watoto wao kupatiwa chanjo katika uzinduzi huo, ambao ni Maria Andrea, Jackline Festo na Eda Tarabani wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuona umuhimu wa kupeleka chanjo kwa ajili ya kupunguza vifo kwa watoto wadogo, huku wakiongeza kuwa wao watakuwa mabarozi wa kutoa Elimu kwa wenzao ili waweze kuwapeleka watoto wao kupatiwa chanjo kwa kuwa huduma hiyo ni bure.
Sanjari na hayo, pia wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuwapelekea Magari mawili ya kubebea wagonjwa kwani yatasaidia kwa baadhi ya wagonjwa ambao wanaishi umbali mrefu kwa kuwa walikuwa wakikosa huduma ya haraka.