Baadhi ya wafanyakazi wa mradi wa maji na usafi wa mazingira unaotekelezwa na kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi katika kata ya Mnara na Mandwanga Halmashauri ya Mtama wilayani Lindi,wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga(hayupo pichani)wakati akifunga kikao kazi cha wadau wa maji .
Meneja mradi wa maji na usafi wa mazingira unaotekelezwa na kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi Method Kamuhanda,akitoa taarifa ya ujenzi wa miradi ya maji katika kata ya Mnara na Mandwanga Halmashauri ya wilaya Mtama mkoani Lindi,katikati ni mhandisi wa maji wa Doyasisi hiyo Olaph John.
Mkuu wa wilaya ya Lindi mkoani Lindi Shaibu Ndemanga kushoto,akipokea taarifa ya ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Doyasisi ya Masasi Joyce Liundi kulia, katikati ni msaidizi wa Askofu wa kanisa hilo Douglas Msigala.
Na Mwandishi wetu Mtama,
MKUU wa wilaya ya Lindi mkoani Lindi Shaibu Ndemanga,ameuagiza wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wafungia mita za malipo ya kabla(Pre paid) wananchi waliounganishiwa huduma ya maji ili kuongeza mapato ya serikali.
Alisema,mita hizo zitasaidia kudhibiti upotevu wa maji na zitawawezesha wananchi kununua na kupata huduma ya maji akiwa sehemu yoyote bila kufika kwenye mita na zitakomesha malalamiko ya kubambikiwa ankara za maji.
Ndemanga amesema hayo jana,wakati akifunga kikao kazi cha wadau wa sekta ya maji baada ya ziara ya siku tatu ya kutembelea ujenzi wa miradi maji ya Mandwanga-Lindwandwali,Kiuta-Mikongi na Nyundomoja-Nambau inayotekelezwa na Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi.
Amezitaka taasisi zinazohusika na sekta ya maji wilayani humo,(Ruwasa na mamlaka ya maji) kuzihamasisha taasisi za umma na binafsi kuunganisha maji kwenye taasisi zao ili ziweze kuongeza mapato yake, badala ya kuziacha zinapata maji kupitia vituo maalum vilivyojengwa kwa ajili ya wananchi.
Ndemanga,amewashukuru wadau Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi kupitia mradi wa maji na usafi wa mazingira kwa kutenga zaidi ya Sh.bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji na huduma nyingine katika vijiji mbalimbali ambayo itawezesha wananchi kupata huduma bora za kijamii.
Alisema,fedha zilizotolewa na kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi kutekeleza miradi ya maji katika kata ya Mnara na Mandwaga zingeweza kupelekwa katika wilaya na mikoa mingine hapa nchini.
Amewataka wataalam wilayani Lindi,kuwashirikisha wananchi pale wanapotaka kuanzisha miradi ya maendeleo na kuepuka kufanya shughuli zao kwa kificho ili kuepuka malalamiko ya wananchi.
Aidha,amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote katika wilaya ya Lindi(Mtama na Halmashauri ya Manispaa Lindi)kuwatumia mafundi wenye ujuzi pindi wanapojenga miradi ikiwemo madarasa,mtundu ya vyoo na majengo mengine ya umma na kuacha kuwatumia mafundi wa mitaani ili kuepuka miradi kujengwa chini ya kiwango.
Msaidizi wa Askofu wa kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi mchungaji Douglas Msigala alisema,Kanisa Anglikana litaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na serikali katika kuboresha huduma za kijamii bila kujali itikadi za dini,rangi au kabila.
Hata hivyo,ameiomba serikali kushirikiana na kanisa hilo katika ulinzi wa miradi inayotekelezwa na kanisa hilo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na isaidie kuboresha maisha ya wananchi hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini.
“wananchi na watendaji wa serikali tunwaomba sana wawe waaminifu na waadilifu katika ujenzi na uendeshaji wa miradi inayotekelezwa na wadau wakiwemo sisi kanisa Anglikana ili miradi hiyo ijengwe kwa viwango na kuleta tija kwa wananchi”alisema.
Katibu wa Kanisa Anglikana Doyasisi ya Masasi Joyce Liundi alisema,mradi wa maji Mandwanga na Mnara katika Halmashauri ya Mtama unatekelezwa na Doyasisi hiyo chini ya usimamizi wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) na utahudumia zaidi ya wananchi 26,532 wa vijiji 10.
Alisema,mradi ulizinduliwa rasmi mwezi Juni 2023 na shughuli za utekelezaji ikiwemo ujenzi wa miundombinu zilianza mwezi Agosti baada ya kukamilika taratibu za manunuzi na unatekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 3,792,063,005.
Kwa upande wake Meneja mradi wa maji na usafi wa mazingira(Wash Project) Method Kamuhanda alisema, ujenzi wa miradi hiyo umefikia zaidi ya asilimia 85 na inatarajia kukamilika mwezi Machi mwaka huu.
Ametaja kazi zilizotekelezwa ni uchimbaji wa mitaro na kulaza bomba mabyo imefanyika kwa kushirikiana na wananchi,ujenzi wa matenki ya kuhifadhi maji, kujenga ofisi ya jumuiya ya watumia maji (CBWSO),nyumba za mashine(Pump House) na kufunga umeme jua katika kijiji cha Mandwanga.
Pia alisema,katika utekelezaji wa mradi huo suala la usafi wa mazingira linapewa nafasi kubwa ambapo wametoa elimu na kuunda vikundi vya kuweka,kukopa na kuanzisha miradi ya kujiingizia kipato ili kukuza uchumi wa kaya na kutoa mafunzo ya mtazamo chanya na kuwajengea uwezo wa kutambua fursa zilizopo katika maeneo yao.
Diwani wa kata ya Mnara Athuman Mpole,ameipongeza Doyasisi ya Masasi kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi ya maji kwa kuishirikisha jamii na serikali,hata hivyo ameiomba kujenga miradi mingine ya maji kwenye vijiji viwili vya kata hiyo ambavyo hakuna huduma ya bomba.
Mtendaji wa kata ya Mandwanga Jenala Wanje alisema,kabla ya kujengwa kwa mradi wa maji Mandwanga-Lindwandwali wananchi walikuwa wanachota maji kwenye madimbwi na wengine kuchota maji barabarani ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Wanje alieleza kuwa,mradi huo utakapokamilika kwa asilimia 100 utawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama na hivyo kupungua kwa baadhi ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama.