Na John Walter-Babati
Watu ambao hawajajulikana hadi sasa wamemshambulia na kumsababishia kifo kijana mmoja anayefahamika kwa jina la Julius Msele (21) ambaye ni dereva bodaboda mjini Babati mkoani Manyara na kupora pikipiki yake.
Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoani Manyara George Katabazi amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo ambapo amesema watu hao walimhadaa dereva bodaboda huyo na mwishowe kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali na kumsababishia kifo katika mtaa wa Maisaka kati pembezoni mwa barabara.
Mwenyekiti wa mtaa wa Maisaka A, Hussein Mkindi anasema wanapanga na mtaa jirani wa Maisaka kati kuunda ulinzi shirikishi wa pamoja ili kudhibiti uhalifu.
Mama wa marehemu Marry Pantaleo, anasema mwanaye ambaye ni kitinda mimba hakuwa na ugomvi na mtu na kwamba alikuwa msaada nyumbani.
‘Pikipiki yake Mwanangu alishamaliza mkataba tangu mwaka jana, hivyo alikuwa akijitafutia ridhiki yake na kuisaidia familia, Nina uchungu Sana, naliomba Jeshi la polisi liwatafute wahusika na hatua za kisheria zifuate” akizungumza Mama huyo kwa Uchungu akibubujikwa na machozi
Baadhi ya madereva boda boda wakiwemo wa kijiweni kwake wanaeleza kuwa walimkuta marehemu akiwa anavuja damu maeneo ya kichwani huku mkononi akiwa ameshika shilingi elfu moja.
Wamesema inawauma Sana kwa kuwa ni tukio la pili la dereva bodaboda kuuawa katika muda na eneo hilohilo, ambapo lingine lilitokea mwaka Jana na pikipiki kuporwa.
Kamanda Katabazi amesema Jeshi hilo linaendelea kufanya msako na upelelezi ili kuwabaini wahalifu hao huku akizungumza na Madereva bodaboda na kuwataka kuwa na umoja lakini pia kusoma alama za hatari mapema ili waweze kujilinda na kutoa taarifa wanapohisi wapo mashakani.