Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani wakimfanyia upasuaji wa kupandikiza mshipa wa damu mgonjwa ambaye mshipa wake ulikuwa umeziba ((Coronary Artery Bypass Graft Surgery – CABG) wakati wa kambi maalumu ya siku nne iliyoanza leo katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 15 wanatarajia kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo
Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakivuna mshipa wa damu kwenye mguu wa mgonjwa utakaopandikizwa katika mishipa ya damu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku nne ya upasuaji mkubwa wa moyo inayofanywa na wataalamu hao kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani
Madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani kumfanyia upasuaji wa tundu dogo mgonjwa ambaye mshipa wake wa damu umeziba wakati wa kambi maalumu ya siku nne ya matibabu ya moyo inayofanyika katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 10 wanatarajia kufanyiwa upasuaji mdogo wa moyo
Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani wakiandaa vifaa vinavyotumika kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba wakati wa kambi maalumu ya siku nne inayofanyika katika Taasisi hiyo.
Picha
Na: Mwandishi Maalumu
Wagonjwa 25 wenye matatizo ya mishipa ya damu kuziba kwa muda mrefu na matatizo ya valvu za moyo kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya siku nne inayofanyika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo inayoenda sambamba na utoaji wa mafunzo ya kubadilishana ujuzi inafanywa na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani.
Katika kambi hiyo wagonwa 10 watafanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab na wengine 15 kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kuzibua mishipa ya damu pamoja na kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery – CABG).
Akizungumza kuhusu kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Dkt. Tatizo Waane alisema upasuaji wa tundu dogo utahusisha wagonjwa wenye matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu kwa muda mrefu na wagonjwa ambao valvu zao za moyo hasa zile za kushoto zimeziba.
Dkt. Waane ambaye pia ni Mkurugenzi wa tiba ya moyo JKCI alisema upasuaji wa tundu dogo utahusisha wanawake kwa wanaume lakini upande wa wanawake wanatarajia kutoa nafasi ya kuzibua valvu za moyo zilizoziba kwa wanawake wanaotarajia kushika ujauzito na kulea watoto kabla ya valvu hizo kubadilishwa.
“Katika kambi hii wanawake ambao valvu zao zimeziba na wapo katika kipindi cha matarajio ya kupata watoto na wagonjwa wengine ambao wakati wao wa kubadilisha valvu bado haujafika watapewa matibabu ya kuzibuliwa valvu hizo na kuendelea kuishi wakiwa vizuri”, alisema Dkt. Waane
Dkt. Waane alisema wagonjwa ambao wamebadilishwa valvu zao za moyo ili kufanya valvu hizo ziweze kufanya kazi vizuri wagonjwa hutumia dawa za kulainisha damu lakini inapofikia mwanamke anataka kupata mtoto dawa hizo huwa si nzuri wakati wa ujauzito.
“Tunapenda kuwafanyia matibabu ya kuzibua valvu za moyo wanawake walio katika kipindi cha kupata watoto kwasababu matibabu hayo yanawapa muda wa kuwa salama kwa kipindi cha miaka 10 hadi 15 kushika ujauzito na kulea na baada ya hapo ndio wanabadilishwa valvu”, alisema Dkt. Waane
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema wagonjwa ambao ni watu wazima wenye matatizo ya mishipa ya moyo kuziba wanatarajia kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo (Bypass Surgery) na wengine watapandikizwa mishipa ya damu iliyovunwa sehemu nyingine za mwili (Coronary Artery Bypass Graft Surgery – CABG).
Dkt. Angela alisema katika kambi hiyo pia watafanya upasuaji mkubwa wa moyo wa kubadilisha mshipa wa moyo mkubwa ambao umetanuka na valvu (Bentall Procedure).
“Kupitia kambi hii tunatamani madaktari wetu wapate mbinu mpya za kutoa huduma za upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa moyo ili tuweze kuwasaidia watanzania ambao wanahitaji huduma hizi”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema matibabu yanayofanyika katika kambi mbalimbali hufanyika pia na madaktari wazawa lakini kupitia kambi hizo wataalamu wanapata mbinu nyingine zaidi za upasuaji wa moyo kutoka kwa wabobezi waliopo ulimwenguni wa upasuaji wa moyo.
Naye mgonjwa anayetarajia kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi hiyo Jackson Mhandu alisema mishipa yake mikubwa miwili ya damu imeziba hivyo kupata changamoto za kuchoka na kushindwa kufanya majukumu yake kama ilivyokuwa awali.
Jackson alisema baada ya kufanyiwa upasuaji anatarajia kurejea katika hali yake na kuendelea na maisha kwani yeye ni baba anayetegemewa na familia yake.
“Nimekuwa nikipata changamoto za kifua kubana, kukosa nguvu, kuchoka mara kwa mara hata nikitembea kidogo tu na hata kushindwa kufanya kazi zangu za kila siku, natarajia baada ya upasuaji hizi changamoto zitaondoka”, alisema Jackson