KAMATI ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), imeipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kuendeleza tafiti na bunifu zinazochagiza usanifu na utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA inayoleta tija kwa taifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya PAC Mh. Japhet Hasunga, mara baada ya kamati hiyo kufanya ziara fupi ya kutembelea Kituo Cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGOVRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kilichopo jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Mh. Hasunga amesema kwamba, e-GA imewezesha serikali kuokoa fedha nyingi kwa kusanifu na kutengeza mifumo ya TEHAMA inayotumika katika taasisi mbalimbali za umma ambapo, hapo awali mifumo hiyo ilinunuliwa kutoka nje ya Tanzania kwa gharama kubwa.
Mh Hasunga amebainisha kwamba, uzoefu unaonesha kuwa katika taasisi mbalimbali za umma walizozitembelea siku za nyuma kulikuwa na changamoto nyingi kuhusu suala la mifumo ya TEHAMA.
“Moja ya jambo lililokuwa linatusumbua sana kamati hii ni taasisi nyingi kununua mifumo ya TEHAMA kutoka nje, lakini msimbo (source code) zinabaki kule kwa waliotengeneza mifumo na wakati mwingine mifumo hiyo baada ya muda haitumiki tena, na hivyo sisi tumekuwa tukisema hakuna thamani ya fedha katika ununuaji wa mifumo hiyo ambayo tumetumia gharama kubwa sana kuinunua,” amefafanua.
Hasunga ameongeza kwamba, licha ya mifumo hiyo kununuliwa kwa gharama kubwa lakini haikuwa na matokeo yaliyotarajiwa hivyo kuziingiza taasisi hizo katika matumizi mabaya ya fedha.
“Kuna taasisi zilinunua mifumo kwa zaidi ya bilioni 30, lakini mfumo haujamaliza mwaka wanautupa, na tulipowauliza walisema waliona mfumo huo haufai hivyo wameamua kutafuta mfumo mwingine,” amebainisha Hasunga.
Ameongeza kuwa katika ziara hiyo kamati imebaini kwamba, e-GA imesaidia kusanifu na kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA nchini, ambayo imezisaidia taasisi za umma kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kununua mifumo kutoka nje ya nchi.
Katika kuhakikisha mifumo ya TEHAMA Serikalini inawasiliana na kubadilishana taarifa, Hasunga ameitaka e-GA kuhakikisha kwamba taasisi nyingi zaidi zinaunganishwa katika Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (GovESB), ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali mtandao kwa wananchi.
“Tumefurahi sana kuona namna mifumo mbalimbali inavyowasiliana, tujitahidi tufike angalau asilimia 80 tu tutakuwa tumefika pazuri kwa sababu tutapunguza gharama na malalamiko katika utoaji wa huduma za serikali mtandao,” ameeleza Mh. Hasunga.
Naye mjumbe wa kamati hiyo, Mh.Ester Matiko, ameipongeza e-GA na kushauri Serikali kuwekeza zaidi kwa vijana ili kuwezesha nchi kuingia katika teknolojia za kisasa ikiwemo ‘blockchain’ na akilii bandia.
“Uwepo wangu hapa nimepata vitu vingi vya ziada ambavyo nilikuwa sivijui, hivyo niiombe Serikali na taasisi zake wawaangalie vijana hawa na wengine ambao wapo huko nje kuhakikisha tunawasaidia na wanatumika ipasavyo katika ujenzi wa Serikali Mtandao,” amesema Matiko.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Ridhiwani Kikwete, ameiomba kamati hiyo kuwa mabalozi wa kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), katika kuhakikisha inakuza jitahada za Serikali Mtandao nchini.
Pia, Mh.Kikwete ameieleza kamati hiyo kwamba kituo hicho cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao kina eneo finyu hivyo, e-GA inahitaji kutengewa bajeti ili kujenga miundombinu (majengo) yake katika eneo la Kikombo.
“Kituo chetu kinatakiwa kipate nafasi kubwa sana, mmejionea wenyewe maabara zetu ni ndogo sana hivyo serikali (Wizara) itakapoleta bajeti huko bungeni tunaomba mlizingatie jambo hili,” ameeleza Kikwete.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba, ameishukuru kamati hiyo kutembelea kituo hicho na kuahidi kutekeleza maelekezo, maoni na ushauri uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo ili kuimarisha bunifu na tafiti za Serikali Mtandao.