Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimwelezea huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipotembelea banda hilo kabla ya kufunga mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo leo katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo mjini Zanzibar
Na: Mwandishi Maalumu – Zanzibar
WIZARA ya afya Zanzibar imelekezwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuhakikisha huduma za upasuaji wa moyo zinaanza kutolewa kwa kipindi cha muda mfupi Zanzibar.
Ushirikiano huo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete umelenga kupunguza athari na matatizo yanayoweza kuhusishwa na kuchelewa kwa matibabu hivyo kuokoa maisha ya wananchi na wageni wanaotembelea Zanzibar wanapokutwa na maradhi ya moyo.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo leo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alisema Serikali ya Zanzibar iko tayari kukuza ushirikiano na kutenga rasilimali zitakazohusika katika utafiti, kinga na matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kuboresha huduma za afya Zanzibar.
“Serikali ya Zanzibar iko tayari kuwekeza rasilimali za kutosha na vifaa vinavyohitajika kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi nyingine zinazotoa huduma za matibabu ya moyo duniani kuifanya Hospitali ya Lumumba kuwa na kitengo cha kuhudumia wagonjwa wa moyo ”,
“Ushirikiano huu utasaidia kujenga uwezo wa ndani na kuhakikisha kuwa wagonjwa wa moyo waliopo Zanzibar wanapata huduma na matibabu ya dharura kwa wakati ili kupambana na vifo vinavyoweza kuepukika”, alisema Mhe. Dkt. Mwinyi
Mhe. Dkt. Mwinyi alisema ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wenye magonjwa ya moyo wanapata faraja, Serikali inatengeneza mkakati wa taifa wa kupunguza matumizi ya vyakula vinavyohusishwa na magonjwa ya moyo ili kutunza afya za wananchi.
“Nchi yetu ina dhamira ya kukuza utalii ikiwemo utalii wa matibabu hivyo Zanzibar ina fursa ya kipekee kwani ikiwekeza miundombinu mizuri, kuwa na vifaa vya kisasa wageni wataweza kuchanganya mapumziko yao na kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya zenye viwango wanapokuwa nchini”, alisema Mhe. Dkt, Mwinyi
Akizungumza kuhusu mkutano huo Mhe. Dkt. Mwinyi alisema ni matumaini yake kuwa mafunzo yaliyopatikana na ushirikiano ulioundwa katika mkutano huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya na kuimarika kwa afya za watu walioathirika na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Kwa hakika kufanyika kwa mkutano huu hapa Zanzibar ni ushahidi kuwa juhudi na ushirikiano uliopo kwa wizara zetu mbili za afya katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi kupitia mbinu ya kubadilishana maarifa na kukuza ufumbuzi katika tafiti mbalimbali”,
Mhe. Dkt. Mwinyi alisema uwepo wa wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi unaonyesha nia ya kitaifa na kimataifa ya kujitolea katika kuendeleza huduma ya kudhibiti magonjwa ya moyo na kutoa matibabu ya magonjwa hayo hapa nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Asha Izina alisema kupitia mkutano huo wataalamu wa afya wameweza kubadilishana uzoefu utakaowasaidia kutoa huduma bora zaidi.
Asha alisema huduma za matibabu ya moyo umekuwa ukihimarishwa kupitia programu mbalimbali kwa wataalamu wa afya lengo likiwa kuzifanya huduma hizo kuwa na adhi sawa duniani.
“Tunaamini wataalamu wa afya walioshiriki katika mkutano wetu walivyokuja na wanavyoondoka wako tofauti kwani wameweza kupata kitu kipya katika fani zao za kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo”, alisema Asha
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema washiriki 100 kutoka Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar wameweza kushiriki mkutano huo uliowawezesha kupata mwanga wa namna ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo.
Dkt. Kisenge alisema kupitia mkutano huo wataalamu wa afya wameweza kujadili maendeleo ya magonjwa ya moyo barani Afrika na kuweka mikakati itakayosaidia wagonjwa hao.
Jumla ya washiriki 500 kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki mkutano wa pili wa kimataifa wa magonjwa ya moyo ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliokuwa na kauli mbiu “Maendeleo katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo Afrika”.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hessein Ali Mwinyi akizungumza na washiriki wa mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo kutoka nchi 30 wakati wa kufunga mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo uliofanyika kwa siku mbili katika Hotel ya Golden Tulip iliyopo mjini Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hessein Ali Mwinyi akimkabidhi ngao mwakilishi kutoka kampuni ya kusambaza dawa za binadamu ya Anudha wakati wa kufunga mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo leo katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo mjini Zanzibar
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimwelezea huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipotembelea banda hilo kabla ya kufunga mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo leo katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo mjini Zanzibar
Daktari wa wagonjwa wa dharura na wanaohitaji uangalizi maalumu anayetoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Said Kilindimo akiwaonyesha wataalamu wa afya namna ya kumhudumia mgonjwa wa dharura wakati wa mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo uliomalizika leo katika Hoteli ya Golden Tulipo iliyopo mjini Zanzibar
Mwakilishi kutoka Kampuni ya kusambaza dawa ya Sun Pharma akiwaelezea wataalamu wa afya waliofika katika banda lake dawa zinazopatikana katika kampuni hiyo wakati wa mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo uliomalizika leo katika Hoteli ya Golden Tulipo iliyopo mjini Zanzibar
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hessein Ali Mwinyi wakati wa kufunga mkutano huo leo katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo mjini Zanzibar