Na. WAF, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI imeipongeza menejimenti na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa kwa ubora wa Huduma na kuwatia moyo kwa kuendelea kuwahudumia wananchi .
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stansilaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya Huduma za kibingwa na bingwa bobezi zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa iliyopo Jijini Dodoma.
Mhe. Nyongo amesema kuwa Hospitali hiyo imekuwa ya mfano katika utoaji wa Huduma bora na usafi wa mazingira na kuleta ufanisi sahihi wa uwekezaji mkubwa ulofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Sluhu Hassan.
“Hongereni kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuwahudumia watanzania lakini pia Mkurugenzi husisite kutuma kutuma vijana wako kuendelea kujifunza ili Tanzania tuzidi kuwa kivutio cha tiba Utalii Afrika mashariki na Afrika nzima kwa ujumla”, Amesema Mhe. Nyongo.
Vile vile ametoa wito kwa uongozi huo kwendelea kuwa wabunifu katika kuongeza mapato ya hospitali hiyo ili kujiimarisha zaidi kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi kwa serikali kuu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika ameishukuru serikali chini ya uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika Hospitali hiyo hususani katika vifaa tiba na vitendanishi, kusomesha wataalamu na upatikanaji wa dawa kwa wakati.