Naibu waziri wa afya Zanzibar Mhe.Hassan Khamis Khafidh akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya ugonjwa wa macho mekundu (red eye) huko Wizara ya Afya Mjini Unguja.

Mratibu wa huduma za afya ya msingi na matibabu ya macho  dkt. Rajab Mohammed Hilal akitoa maelezo ya kitaalam kuhusiana na ugonjwa wa macho mekundu (red eye) huko Wizara ya Afya Mjini Unguja.

PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR

Na Fauzia Mussa,  Maelezo Zanzibar

Jumla ya wagonjwa 4,579 wa ugonjwa wa macho (red eyes) wameripotiwa katika vituo vya afya, na hospitali  Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya  ugonjwa huo huko Wizara ya Afya wilaya ya mjini  Naibu Waziri wa wizara hiyo  Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema idadi ya takwimu hizo zimejumuisha wagonjwa waliofika   kwenye vituo vya afya na hospitali za binafsi na serikali Unguja na Pemba.

Aidha amewataka wananchi kuacha kutumia  dawa za kienyeji  kutibu ugonjwa huo ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza sambamba  na  kuchukua tahadhari za usafi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara ili kujikinga na maradhi hayo .

amesema endapo jamii itaendelea kutumia dawa hizo   kunaweza kuongeza ukubwa wa tatizo hilo hivyo aliwataka wananchi kufika hospitali mara tu wanapoona dalili za ugonjwa huo ili kupata matibabu stahiki  na kwa wakati sahihi.

Hatahivyo aliiasa  jamii kuacha kushikana  mikono  na mtu mwenye maambukizi au kugusa sehemu ya kitu ambacho kimeguswa na mtu huyo,  na kuwataka  kutumia maji baridi kunawia uso mara kwa mara, pamoja  na kujitenga wakati wa kusubiri huduma katika vituo vya afya ili kuepusha maambukizi mapya.

“ni vizuri mgojwa yeyote wa macho asisubiri eneo walilokaa wagonjwa wengine atibiwe chumba maalum kilichotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa namna hiyo na akimaliza matibabu aende moja kwa moja nyumbani ili kupunguza hatari ya maambukizi mapya”alisema naibu Waziri.

Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusiana na ugonjwa huo mratibu wa huduma za afya ya msingi na matibabu ya macho Dkt. Rajab Mohammed Hilal
 amesema ugonjwa wa macho mekundu husababishwa na virusi   wanaoitwa Adenovirus na kupelekea maambukizi ya kirusi kwenye ngozi  nyembamba  inayozunguka gololi la  jicho (conjunctiva) pamoja na kioo (Cornea)  cha jicho.

Aliongeza kwa kusema  ugonjwa  huo   unaambukizwa   kutoka kwa mtu mmoja mwenye ugonjwa huo na kwenda kwa mwengine na kusambaza maambukizi  kwa  haraka sana ndani ya  siku 10 hadi 12.

Alifahamisha kuwa dalili kubwa za ugonjwa huo ni pamoja na jicho kuwa jekundu, kuwasha na kuchomachoma , mifuniko ya macho kuvimba, macho kuogopa mwangaza, macho kutoa matongo matongo meupe au ya njano kuona ukungu kwa uoni wa mbali katika macho, pamoja na  maumivu ya macho.

Alisema miongoni mwa athari za muda mrefu zinazoweza kujitokeza endapo jamii itaendelea kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo ni pamoja kupunguza uoni.

Itakumbukwa kuwa  wiki mbili zilizopita ugonjwa wa macho mekundu (red eye) uliripotiwa katika mikoa ya Tanzania bara na kutokana na maingiliano ya wananchi  ya mara kwa mara  ugonjwa huo umeweza kuingia  visiwani Zanzibar.