Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma imeandika historia ya watoto watatu kupona ugonjwa wa Sikoseli baada ya kuwafanyia matibabu ya upandikizaji wa Uloto.
Hayo yamebainishwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika wakati akitoa taarfa rasmi kwa vyombo vya habari leo jijini Dodoma baada ya mwaka mmoja tangu Hospitali hiyo ifanye Matibabu ya Upandikizaji wa Uloto kumtibu mtoto mwenye Ugonjwa wa Sikoseli
Dkt. Chandika amesema watoto hao hawana maradhi ya Selimundu tena, na kwamba serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza zaidi ya Billioni 3.6 kuwezesha huduma hizo ili kuokoa maisha watanzania.
“Leo ni siku muhimu sana, ninawataarifu watanzania, Afrika na Dunia nzima kwa Ujumla kwamba Watoto tuliyowapandikiza Uloto hawana Ugonjwa wa Selimundu, wana afya njema, na vipimo vimethibitisha hawana ugonjwa huo tena” ameeleza Dkt. Chandika.
Aidha, Dkt. Chandika, amewashukuru wazazi wa Watoto hao, ambao ni Grace Hosea (8), Elisha John (11), na Isack Kedmond (10), kwa kuiamini hospitali hiyo na kuruhusu Watoto wao kuwa wa kwanza kupokea Huduma za Upandikizaji wa Uloto.
Matibabu ya Upandikizaji wa Uloto yanagharimu kati ya Shilingi milioni 55-65, hata hivyo, tafiti zinaonesha kuwa, kumhudumia mtoto mwenye Seilimundu dawa za kupunguza makali ya ugonjwa, fedha hizo zinaweza kukidhi huduma kwa miaka mitano pekee.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga kiasi cha Shilingi Bilioni 1 katika bajeti ya Mwaka huu wa Fedha kwa ajili ya Matibabu ya Selimundu, hakuna hata mzazi mmoja ametoa fedha, gharama zote zimebebwa na serikali” ameshuku Dkt. Chandika.
Akitoa ushuda Mtoto Elisha John (11), kwa niaba ya Watoto wenzake waliyopokea huduma ya kupandikizwa Uloto, amesema changamoto zote alizokuwa nazo zimetoweka.
“Nilikuwa napata shida ya kuumwa kichwa, damu yangu ilikuwa haizidi sita, shuleni nilikuwa simalizi mwezi, lazima nitalazwa wiki nzima, sihudhurii vipindi shule, tangu nimetibiwa sijasikia maumivu yoyote”ameeleza Mtoto Elisha.
Kwa mujibu wa Mzazi wa Elisha, kumhudumia mtoto mwenye Sikoseli ni kujitoa sadaka, ambapo mzazi mmoja alilazimika kuacha kazi ili kuwa karibu na mtoto wao.
“Kupata wiki moja ya kutokuugua kwake lilikuwa jambo la muujiza, kwa miaka hiyo 11 ya kuugua kwake, ilibidi mama yake aache kujishughulisha na shughuli za kiuchumi, kwa sababu Ugonjwa huo hauna muda maalumu, hali ingeweza kubadilika muda wowote” alisema Joseph John.
Mbali na Shukrani kwa BMH na Serikali kwa nafuu aliyoipata mtoto wake, ametoa wito kwa serikali kuangalia uwezekano wa kujenga Hosteli Jirani na Hospitali hiyo, ili kusadia familia zinazotoka nje ya Dodoma kufuata huduma hiyo BMH.
Wito huo uliungwa mkono na Profesa, Cornell Uderzo, Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Upandikizaji Uloto kutoka Shirika la Help 3 la nchini Italia, Washirika wa BMH katika huduma za Upandikizaji wa Uloto, kwa kusema kuwa hitaji la Hosteli ni Muhimu si tu kwa BMH, bali ni protokali ya matibabu hayo.
“Kote duniani, si hapa pekee, kunakuwa na makazi ya familia Jirani na Hospitali, kuziwezesha familia kukaa angalau kwa miezi 3 baada ya kuruhusiwa kutoka wodini, kuruhusu madaktari kumfuatili mgonjwa kwa karibu, ikiwa kuna changamoto yoyote, hasa maambukizi” alisema Profesa Uderzo.
Tanzania inashika nafasi ya nne duniani kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa Selimundu, ni ya 3 kwa nchi za Afrika, huku idadi ya Watoto 11,000 wakikadiliwa kuzaliwa na ugonjwa huo kila mwaka, ambapo asilimia 50 hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka 5.
Hospitali ya Benjamin Mkapa ilianza kutoa huduma za Upandikizaji wa Uloto mwaka jana, ikiwa ya kwanza kutoa huduma hiyo kwa nchi za Afrika Mashariki na kati, hadi sasa Watoto 7 wamenufaika na huduma hiyo, huku wengine tisa wakiwa katika mlolongo wa matibabu.