Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii [NSSF] linamshikilia mtuhumiwa Pius Komba [70] mkazi wa Itigi Jijini Mbeya kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya utapeli na kughushi nyaraka mbalimbali.
Mtuhumiwa alikamatwa Januari 25, 2024 eneo la Retco Jijini katika msako wa pamoja uliofanywa na Jeshi la Polisi na Maafisa wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii na kufanikiwa kumtia mbaroni kinara wa kuandaa nyaraka na mihuri bandia na kuwapa wanachama wa NSSF ili wapate mafao kinyume na sheria inayosimamia ulipwaji wa mafao.
Mtuhumiwa amekuwa akishirikiana na wanachama wa mfuko na baadhi ya maafisa rasilimali watu wa makampuni wanayofanyia kazi kufanya udanganyifu wa taarifa zinazohitajika ili kulipa mafao kwa mujibi wa sheria ya NSSF sura ya 50 marejeo ya mwaka 2018 kifungu 72 (1) (a) (b)
Siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la vishoka/matapeli ambao wamekuwa wakiandaa nyaraka (barua za kuachishwa kazi) za kughushi ambazo hutengeneza na kuwapa wanachama wa mfuko kwenda kufungua madai kinyume na taratibu ambazo ziko wazi kuwa ili mwanachama apate mafao ni lazima awe ameachishwa kazi na anakidhi vigezo vilivyopo kwa mujibi wa sheria.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili akiwemo raia wa nchini Rwanda Assouman Gahigiro [48] na Winny Bruno [31] mkazi wa Kiwira Wilaya ya Rungwe kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bhangi kilogramu 20.
Watuhumiwa walikamatwa Januari 27, 2024 katika kizuizi cha Polisi cha Kayuki kilichopo barabara kuu ya Kyela – Tukuyu ambapo watuhumiwa walikuwa abiria kwenye gari iliyokuwa ikitokea Kyela kuelekea Mbeya Mjini, Askari waliokuwepo eneo hilo walilisimamisha gari hilo na kufanya ukaguzi na ndipo walibaini Bhangi iliyokuwa imefichwa kwenye vifungashio vya Nylon na kuwekwa ndani ya begi la nguo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na upelelezi kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji ili kubaini uhalali wa mtuhumiwa Assouman Gahigiro kuwepo nchini wakati taratibu nyingine za kumfikisha mahakamani kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya zikiendelea.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mkazi wa Mbezi Jijini Dar es Salaam Maulusi Samweli @ Mtui [35] kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali meno mawili ya Tembo yenye uzito wa kilogramu 10 bila kuwa na kibali.
Mtuhumiwa alitiwa mbaroni Januari 27, 2024 katika msako uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi [TANAPA] katika Kijiji cha Mlungu kilichopo Kata ya Miyombweni, Wilaya ya Mbarali na kumkamata mtuhumiwa akiwa ameficha meno hayo kwenye mfuko wa sandarusi akiwa kwenye harakati za kutafuta wateja.
Upelelezi uliofanywa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ni mwindaji haramu, msafirishaji na muuzaji wa nyara za serikali, atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Imetolewa na:
BENJAMIN KUZAGA – ACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.