Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson akifungua Wiki wa Sheria Januari 27, 2024 inayofanyika jijini Dodoma kuanzia Januari 24-30, 2024.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Dodoma Bw. Jackson Kanyerinyeri (aliyeva fulana nyeupe) akifafanua jambo kwa wananchi waliotembelea banda la Mabaraza ya Ardhi na Nyumba wakati wa uzinduzi wa Wiki wa Sheria inayofanyika jijini Dodoma kuanzia Januari 24-30, 2024.
Afisa Ardhi Bi. Anjela kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (aliyevaa miwani kushoto) akitoa maelezo kwa wageni waliotembelea banda la Mabaraza ya Ardhi na Nyumba wakati wa uzinduzi wa Wiki wa Sheria inayofanyika jijini Dodoma kuanzia Januari 24-30, 2024. Wa kwanza kushoto ni Afisa Usajili Msaidizi kutoka Wizara hiyo Bi. Rehema Ndelwa.
Na Eleuteri Mangi, WANMM
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba imeshiriki uzinduzi wa Wiki ya Sheria jijini Dodoma yakiongozwa na Mhe. Dkt. Tulia Ackson Spika wa Bunge la Tanzania.
Uzinduzi huo umefanyika Januari 27, 2024 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma ukitanguliwa na matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria ambao umehusisha viongozi mbalimbali wa mahama, watumishi wa umma na wananchi kutoka jiji la Dodoma.
Akizungumzia ushiriki wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Dodoma Bw. Jackson Kanyerinyeri amesema kuwa moja ya jukumu lao ni kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda hilo katika masuala ya ardhi, migogoro ya ardhi namna inavyotatuliwa katika mabaraza hayo hadi kutolewa hukumu.
Bw. Kanyerinyeri ameongeza kuwa wamepata wasaa mujarabu wa kuwaeleza wananchi juu ya mabadiliko ya Sheria Na 3 ya 2021 ambayo imeondoa mamlaka ya mabaraza ya Kata kusikiliza kesi za migogoro ya ardhi badala yake mabaraza hayo yana jukumu la kusikiliza na kusuluhisha migogoro baina ya wananchi ikishindikana migogoro hiyo iwasilishwe Baraza la Ardhi na nyumba la wilaya na kupewa cheti ndani ya siku 30.
Aidha, Bw. Kanyerinyeri ameongeza kuwa wanaendelea kuwasistiza wananchi wamalize migogoro ya ardhi kwa nyia ya mazungumzo na mapatano hatua inayookoa muda, kuondoa uhasama na inawapa wananchi muda wa kufanya shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Wiki ya Sheria 2024 imeanza Januari 24 na inatarajiwa kuhitimishwa Januari 30 yakiongozwa na kaulimbiu “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai”