NA VICTOR MASANGU, PWANI
Serikali Mkoani Pwani katika kumuunga mkono Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati kabambe ya kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo cha kisasa na chenye tija ambacho kitajumuisha mazao ya kibiashara kwa lengo la kukuza uchumi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge wakati wa halfa fupi ya kukabidhi matreka matatu kwa uongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Kibaha vijijini.
Kunenge alisema kwamba matreka hayo matatu ambayo wamepatiwa na Rais Samia yatakwenda kuwa msaada mkubwa na kuleta mapinduzi katika kilimo cha kisasa.
“Sisi kama Mkoa wa Pwani kwa sasa tumejipanga kuhakikisha kwamba tunajikita zaidi katika kuboresha sekta ya kilimo na kwa sasa tumepokea matreka haya kwa ajili ya halmashauri ya Wilaya ya Kibaha vijijini kwa hivyo hatuna budi kumshukuru Rais wetu kwa hatua hii ya kutupatia matreka haya,”alisema Kunenge.
Aidha Kunenge alibainisha kwamba kwa sasa wameshaanza kujikita katika kilimo cha mazao ya biashara ikiwemo zao la Pamba,ufuta kilimo pamba.mchikichi,korosho mihogo pamoja na mazao mengine ambayo yataweza kuleta mabadiliko katika kukuza shughuli mbali mbali za kiuchumi.
Aidha aliongeza kwamba Mkoa wa Pwani wanataka kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo hivyo ana imani kubwa mabadiliko hayo yatakwenda katika halmashauri zote tisa zilizopo katika Mkoa wa Pwani.
Pia kunenge aliwaomba viongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha kwamba wanayatunza vizuri matrekta hayo ili yaweze kudumu kwa kipindi kirefu ili kuweza kuwasaidia wakulima katika kilimo cha biashara.
Aidha pamoja na hayo aliongeza kwamba katika kuendana na kasi ya mabadiliko katika Wilaya ya Rufiji tayari kumeshafanyika uzinduzi wa zao la pamba na kwamba kutajengwa kiwanda kikubwa kwa ajili ya kuchakata zao hilo.
Kunenge amempongeza kwa dhati Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za hali na mali katika kukuza sekta ya kilimo cha kuwezesha matreka hayo.
Aidha Kunenge katika hatua nyingine aliwawahimiza wakulima wa Mkoa wa pwani kuendana na mabadiliko na kuwataka wakulima wajikite zaidi katika kilimo cha mazao ya biashara.
Sambamba na hayo alisema wapo katika mikakati ya kujenga skimu kubwa za umwagiliaji ambazo zitaweza kuwasaidia wakulima katika kuendesha shughuli zao za kilimo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amesema kwamba wameshakubaliana matrekta hayo yatakwenda katika halmashauri ya Wilaya ya kibaha ili kuboresha kilimo cha kisasa.
Aidha alibainisha kwamba katika mpango wao wamekubaliana mambo matatu ikiwemo kuunganisha kilimo pamoja na viwanda,rasirimali watu pamoja na teknolojia lengo ikiwa ni kuwasaidia wakulima kulima kilimo cha kisasa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha vijijini Erasto Makala lengo lao kubwa ni kutoka katika kilimo cha chakula na kujikita katika biashara.
Mkoa wa Pwani kwa sasa umejipanga kuunganisha kilimo pamoja na viwanda lengo ikiwa ni kutimiza azma ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hasssan kulisha dunia nzima kupitia sekta ya kilimo.