Na John Walter-Manyara
Klabu ya waandishi wa habari Manyara imeendesha mdahalo wa tatu ulioshirikisha Jeshi la polisi kwa lengo la kuimarisha usalama kwa waandishi wa habari wanapokuwa kwenye majukumu yao.
Akifungua mdahalo huo uliofanyika mjini Babati Januari 23,2024, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Manyara George Katabazi, amewataka Waandishi wa habari kuandika habari zao kwa ufanisi ili zilete mabadiliko katika maeneo mbalimbali ikiwemo suala la ukatili wa kijinsia lililoshamiri mkoani hapa na kwamba suala la ulinzi na usalama ni uhakika.
Amesisitiza ushirikiano zaidi na Jeshi la polisi na uandishi usioegemea upande mmoja utaleta ufanisi mzuri wa kazi na kusaidia kupunguza upotoshaji na taharuki kwa jamii.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari mkoani Manyara Zacharia Mtigandi, amesema lengo la mdahalo huo ni kuboresha mahusino mazuri baina ya jeshi la polisi na waandishi wa habari.
Hata hivyo Mtigandi amesema, Jeshi la polisi mkoani Manyara limeendelea kushirikiana na waandishi wa habari mkoani humo katika utendaji wa kazi.
Kwa mujibu wa data zilizopo Mkoa wa Manyara una kiwango kidogo Cha madhila,matukio matatu pekee yamerekodiwa mwaka 2022 ikilinganishwa na mikoa Mingine.