Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akielezea umuhimu wa usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha, wakati wa kutoa elimu ya fedha kwa vitendo kwa njia ya sanaa katika Mtaa wa Malikula Chamwino mkoani Morogoro.
Mtaalamu wa masuala ya fedha wa Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyanza, akifafanua kuhusu kuwatumia wahamasishaji wa elimu ya fedha waliosajiliwa ili kuwa na elimu sahihi, wakati wa kutoa elimu ya fedha kwa vitendo kwa njia ya sanaa katika Mtaa wa Malikula Chamwino mkoani Morogoro.
Mtaalamu wa masuala ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Msumule (katikati) na Debora Mlimba kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI), wakitoa zawadi ya mfuko kwa Bw. Sijali Omar Mogela, mkazi wa mtaa wa Malikula Chamwino mkoani Morogoro, baada ya kujibu kwa ufasaha maswali yaliyotokana na elimu ya fedha iliyotolewa na wasanii kutoka TACCI.
Mtaalamu wa masuala ya huduma ndogo za Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Msumule (katikati) na Debora Mlimba kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI), wakitoa zawadi ya mfuko kwa Bi. Hadija Haji, mkazi wa mtaa wa Malikula Chamwino mkoani Morogoro, baada ya kujibu maswali yaliyotokana na elimu ya fedha iliyotolewa na wasanii kutoka TACCI.
Wasanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI), wakitoa elimu ya fedha kwa njia ya sanaa kwa wakazi wa mtaa wa Malikula Chamwino mkoani Morogoro.
Wakazi wa mtaa wa Malikula Chamwino mkoani Morogoro, wakifuatilia igizo kuhusu namna ya kusajili vikundi vya kijamii vya huduma ndogo ya fedha, kutoka kikundi cha Sanaa cha Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI) (hawapo pichani)
Kikundi cha Ngomma kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI) kikitumbuiza kabla ya kuanza kutoa elimu ya Fedha kwa Wakazi wa mtaa wa Malikula Chamwino mkoani Morogoro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Morogoro)
Na. Peter Haule, WF, Morogoro
Wizara ya Fedha kupitia Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji Elimu ya Uraia (TACCI) wamefanikiwa kuwafikishia elimu ya Fedha baadhi ya wakazi wa Morogoro kwa njia ya Sanaa ikiwa ni mwanzo wa mkakati wa kufikisha elimu hiyo nchi zima ili kutekeleza Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.
Akizungumza baada ya elimu hiyo iliyotolewa mtaa wa Malikula Chamwino, mkoani Morogoro, Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alisema kuwa elimu kwa njia ya Sanaa mkoani Morogoro ni mwanzo wa matukio kama hayo yatakayofanyika nchi nzima hususan maeneo ya vijijini kwa kuwa njia hiyo imeonesha mafanikio makubwa.
“Lengo kubwa ni kufika vijijini ambako kuna uelewa mdogo wa masuala ya elimu ya Fedha na tutajitahidi kuchagua maeneo mahususi ambayo yameainishwa kwenye utafiti wa FISCOPE wa mwaka 2023 ambao unaonesha ujumuishwaji mdogo wa masuala ya fedha unaochangiwa na uelewa mdogo”, alieleza Bw. Kimaro.
Kwa upande wake Mtaalamu wa masuala ya Vikundi vya Kijamii vinavyotoa Huduma Ndogo za Fedha, Bw. Joseph Msumule, alisema kuwa muitikio wa wananchi kujitokeza kwa wingi kusikiliza elimu ya fedha kumechangiwa na Sanaa ya maigizo na ngoma iliyofanywa kwa weledi mkubwa ikilenga elimu ya fedha kwa njia rahisi.
Alisema maigizo hayo yalilenga kuweka akiba, uwekezaji, mifuko ya hifadhi ya jamii, usimamizi binafsi wa masuala ya fedha na namna ya kusajili vikundi ili kuepusha wananchi kudhulumiwa na kukopa maeneo ambayo hayajaainishwa katika Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha.
Kwa upande wao wananchi wa mtaa wa Chamwino Morogoro, wameipongeza Wizara kwa kuwapelekea elimu ya fedha kwa njia ya sanaa kwa kuwa inawarahisishia kuelewa na wapo tayari kuanza kuifanyia kazi kwa kuwashinikiza viongozi wa vikundi vya Kijamii vya Huduma ndogo za Fedha (CMG) kujisajili kwa mujibu wa Sheria.
Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha unalengo la kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025 asilimia 80 ya wananchi wawe na uelewa wa kutosha wa elimu ya fedha.