Kifaa cha kisasa cha ultra sound kinachotembea kumfutata mgonjwa alipo hasa wodini .
Na Lucas Raphael,Tabora
WAKAZI wengi katika Halmashauri ya Mji Nzega Mkoani Tabora wanakabiliwa na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa ambapo kila mwezi zaidi ya wagonjwa 1,300 hupokelewa hospitalini .
Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt Anna Chaduo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili aliyetembelea hospitali hiyo ili kujionea hali ya utoaji huduma za afya kwa jamii.
Alisema kuwa maboresho makubwa ya miundombinu katika hospitali hiyo na vituo vyote vya kutolea huduma za afya yamewezesha huduma za afya kuboreshwa kwa kiasi kikubwa katika halmashauri hiyo ikiwemo kuhudumia magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa.
Alibainisha kuwa huduma zote sasa zinatolewa katika hospitali hiyo na wagonjwa wote wanaofika hapo kutoka katika vijiji mbalimbali wanahudumiwa ipasavyo pasipo tatizo lolote.
Dkt Anna alifafanua kuwa kwa sasa wagonjwa wengi wanaofika hospitalini hapo ni wale wenye magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa ikiwemo mafua makali, kikohozi na moyo ambayo yamekuwa yakisumbua watoto wadogo hadi watu wazima wenye umri wa miaka 60 na kuendelea.
Alitaja chanzo kikubwa cha magonjwa hayo kuwa ni uwepo wa migodi mingi ya madini katika maeneo jirani ambayo hupelekea wananchi kuvuta hewa yenye vumbi na kemikali hivyo kupata athari za kiafya.
Alitaja ugonjwa mwingine ambao umekuwa tishio kwa wananchi kuwa ni malaria kwani wamekuwa wakipata wagonjwa wengi wenye vijidudu vya malaria, hivyo akashauri jamii kujenga utamaduni wa kutumia vyandarua.
‘Wananchi wanaokabiliwa na magonjwa ya njia ya hewa wamekuwa wakiongezeka kila siku sababu kuu ikiwa ni uwepo wa migodi mingi ya machimbo ya dhahabu na vito vingine’’alisema Dkt Anna
Dkt Anna aliongeza kuwa wagonjwa wa malaria nao wamekuwa wakiongezeka katika kipindi hiki cha mvua kutokana na madimbwi mengi kujaa maji na kupelekea mbu kuzaliana kwa wingi ambapo kwa mwezi hupokea takribani wagonjwa 2,300 wa malaria.
‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kiasi cha sh mil 300 mwaka jana kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dharura ili kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa aina zote’, alisema.
Alibainisha kuwa jengo hilo ambalo limekamilia kwa asilimia 100 na kuwekewa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya wagonjwa limekuwa msaada mkubwa sana katika kukabiliana na ongezeko la wagonjwa.
Alitaja huduma ambazo awali zilikuwa hazipatikani lakini sasa zinapatikana kuwa mionzi (x-ray na ultra sound) na sasa unafungwa mtambo wa kuzalisha hewa ya oksijeni.
Akizungumza na gazeti hili mkazi wa Mtaa wa Parking, Tanasha Haruna alisema kujengwa kwa jengo la dharura lenye vifaa vya kisasa kumewarahishia upatikanaji huduma kwa kuwa wagonjwa hawakai foleni tena kama ilivyokuwa huko nyuma.
Aidha aliwashukuru watoa huduma katika hospitali hiyo wakiwemo wauguzi na madaktari kwa kufanya kazi yao kwa weledi mkubwa katika kila kitengo ikiwemom kujali wagonjwa.
Jengo la dharura katika hospital ya mji wa nzega mkoani Tabora lina vifaa vya kisasa linatoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa nje na ndani katika mji huo .
Mganga Mkuu wa Hospitali ya mji wa nzega Dkt Anna Chaduo akitoa maelezo kwa waandishi wa habari juu ya matumizi ya kifaa ultra sound kinavyofanya kazi kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali kwa ajili ya huduma hiyo .
Kifaa cha kisasa cha ultra sound kinachotembea kumfutata mgonjwa alipo hasa wodini .