Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akifungua kikao kazi cha Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha muungano kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (mbele) wakiwa kwenye kikao kazi na baadhi ya watendaji wa Serikali ya Muungano kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kikao kazi hicho kilikuwa na lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha muungano.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mohammed Aboud akichangia hoja wakati wa kikao kazi cha Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha muungano, kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. Waziri huyo ndiye mwenye dhamana ya kushughulikia masuala ya muungano.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akizungumza katika kikao kazi cha Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha Muungano kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
……………………..
Na James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman wamefanya kikao kazi kujadili namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma kwa umma pamoja na kuimarisha Muungano ili uendelee kuwa na tija kwa wananchi.
Akifungua kikao kazi hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amesema pamoja na kujadili masuala ya kuboresha huduma pia kililenga kuimarisha muungano ili kuwaenzi kwa vitendo waasisi wa taifa letu Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, katika kikao kazi hicho wameweza kubadilishana uzoefu wa namna ya kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi wa pande zote mbili za muungano ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema wao kama mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wanataka ushirikiano wa taasisi zinazoshughulikia masuala ya kiutumishi na utawala bora uendelezwe kwa vitendo kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Mhe. Suleiman amesisitiza kuwa, ushirikiano huu una manufaa katika kuboresha huduma zitolewazo na taasisi za umma kwa wananchi na una tija katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Taasisi za Umma nchini.
Mhe. Suleiman amewataka wajumbe wa kikao hicho, kuhakikisha misingi madhubuti ya kiutendaji iliyojengwa katika kikao kazi hicho inaimarishwa ili utekelezaji wake uwe wa vitendo na uweze kuwa chachu ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Masuala yaliyojadiliwa katika kikao kazi hicho kudumisha ushirikiano katika masuala ya Ajira, Serikali Mtandao, Udhibiti wa rushwa, Usimamizi wa Maadili ya Viongozi, Mafunzo kwa Watumishi wa Umma, Utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Utumishi wa Umma, Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma, Uandaaji wa Miundo na Mifumo ya Taasisi na Utawala Bora kwa ujumla.