Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Dkt.Sebastian Pima akizungumza kwenye kikao cha kamati ya afya
Ofisa usafi na Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Desderius Polle
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wananchi Mkoani Mwanza wametakiwa kuchukua tahadhari mbalimbali ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka,kuacha uuzaji wa vyakula holela katika maeneo yasiyo rasmi hatua itakayosaidia kijikinga na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Ra hiyo ilitolewa Jana Jumanne Januari 9, 2024 na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Dkt. Sebastian Pima katika kikao cha kamati ya Afya ya Halmashauri hiyo.
Dkt.Pima amesema Januari 4 mwaka huu walipokea watu wawili walikuwa na dalili za ugonjwa wa kipindupindu ambao walitokea Mkoa wa Simiyu.
“Watu hao walifika kwenye Kituo chetu cha afya Igoma wakitokea Simiyu sehemu wanapochukulia mizigo,na walipofika tukawaona wanadalili ya ugonjwa wa kipindupindu hivyo tukachukua sampuli na tulipo Pima tulibaini kuwa wana ugonjwa huo baada ya majibu tuliwapeleka kwenye kituo chetu cha Mkuyuni”, amesema Dkt.Pima
Baada ya visa hivyo viwili viliendelea kutokea visa vingine viwili eneo la Mkolani huku visa vitatu vikitokea Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
“Hadi sasa tumeishapata wagonjwa saba ambao walilazwa ambapo wawili wa awali tumeisha waruhusu na hali zao zinaendelea vizuri na kwenye kituo chetu cha matibabu tunawagonjwa watano ambao bado wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri”, amesema Pima
Dkt.Pima ameeleza kuwa wanaendelea kufanya ufatiliaji kwa familia mbalimbali waliokutana na wagonjwa hao lakini hawajaonesha dalili za ugonjwa huo.
Ameeleza kuwa ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia ya kula chakula,kunywa maji au kitu chenye vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu na ndio maana wanahamasisha jamii kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni wakati wa kutoka kujisaidia.
Kwa upande wake Ofisa usafi na Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Desderius Polle, amesema mkakati walionao ni kuhakikisha mazingira yote yanaimarishwa ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa kushirikiana na vikundi au Kampuni za usafi katika Halmashauri ya Jiji hilo.
Nae Mwenyekiti wa Wahudumu wa afya ngazi ya Jamii (CHWS) Nyamagana Yohana Wanga, ameshauri nguvu zielekezwe mashuleni kwani Kuna mama ntilie ambao wanawauzia chakula ili wazingatie suala zima la usafi