Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge amefafanua kuwa, Mkoa huo una malengo ya kuandikisha wanafunzi wa shule za awali 55,771 pamoja na wanafunzi 51,446 wa darasa la kwanza.
Ameeeleza, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2023 Jumla ya wanafunzi 25,136 wameandikishwa ikiwa ni sawa na asilimia 45.1 .
Akitoa taarifa hiyo katika kikao cha mtandao cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI ambapo alisema mkoa huo, una malengo wa kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 51,446 ambapo hadi sasa wanafunzi 37,694 wameshaandikishwa, sawa na asilimia 73.3 .
Alieleza, uandikishaji wa shule za awali na darasa la kwanza unaendelea hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2024.
Vilevile akibainisha kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2024, alisema kwa shule za kutwa na shule Teule ya Mkoa ni 40,796 na ufaulu ukiwa ni asilimia 83.7.
Kunenge alieleza, wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wataendelelea na masomo yao bila ya kikwazo chochote.
Kwa upande wa Miundombinu, Kunenge alieleza, mkoa umepokea jumla ya sh. Bilioni 29.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu.
“Ujenzi wa shule mpya 36 ,Vyumba vya madarasa 198,nyumba za walimu 13 matundu ya vyoo 269 ,mabweni 21 vituo vya walimu TRC 13 zitajengwa” Fedha hizi zimekuja kupitia miradi ya Boost, Sequip one na two kutoka Serikali Kuu, Barrick na wadau wengine”
Kuhusu miradi ya Boost ,Kunenge alisema mkoa ulitakiwa kujenga shule 13 ambapo baadhi ya shule zimekamilika .
Kwa upande wa miradi ya Sequip shule zipo 23 na shule 19 kati ya hizo zimesajiliwa na shule nne zinatarajiwa kusajiliwa mwishoni mwa Januari 2024.