Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waganga wa tiba asili.
Waganga wa tiba asili wakiwa ukumbini
Waganga wa tiba asili wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Wilbrod Mutafungwa.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wakati waganga wa tiba asili wakiomba Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu, kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa amewataka waganga hao kushirikiana na Jeshi la Polisi kwenda Kuzuia matukio ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina, migogoro ya ardhi, mauaji ya kujichukulia sheria mkononi, wizi pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Akizungumza Disemba 21, 2023 kwenye mkutano wake na waganga wa tiba asilia zaidi ya 500 katika ukumbi wa kihistoria wa Mahatma Gandhi mkoani humo, Kamanda Mutafungwa amewataka wataalamu hao kwenda kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka ili kuhakikisha wanapunguza matukio ya mauaji na uhalifu.
“Tunatamani kuona uharifu unaisha katika Mkoa wa Mwanza ili ifike hatua matukio ambayo yanakuwa yakileta hofu katika jamii yetu yanaisha mfano mauaji ya kutokana na imani potofu za kishirikina, migogoro ya ardhi, matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto, kuwania mali, unyanganyi, wizi, pamoja na utapeli na ndio maana tumewaita leo ili kuzungumza na kuona namna gani mnaweza kusaidia katika kupunguza vitendo hivyo kwa sababu nyie ni kundi muhimu,” amesema kamanda Mutafungwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, mrakibu mwandamizi wa Polisi (SSP) Yesaya Sudi amewaasa waganga wa tiba asilia kuwafichua waganga bandia wa tiba asilia na wapiga ramli chonganishi katika jamii kwani wao ndio wamekuwa chanzo cha kuchafua sifa ya taaluma hiyo.
“Niombe kwenye eneo hilo ukibaini mtu ambaye anapiga ramli chonganishi usimuache salama kwa sababu atakuwa anachafua kundi lenu pia mkiona mtu hana cheti wala taaluma ya tiba hiyo toa taarifa mapema ili asije kuwachafulia kundi lenu” amesisitiza mwandamizi Sudi
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asilia Mkoa wa Mwanza, Shabani Ramadhani akizungumza kwa niaba ya kundi hilo ametoa wito kwa waganga wenzake kutoa taarifa ya waganga wale wasiofuata sheria huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Hospitali za Rufaa kuwa na kitengo cha tiba asilia.
“Niwaombe waganga wenzangu wa tiba asilia tusivunje sheria za nchi, tuendelee kujiendeleza kusoma katika vyuo vya waganga wa tiba asilia lakini kwa upande wa Serikali na Jeshi la Polisi kuzidi kutoa elimu hii na wasiishie mjini tu bali pia waende hata vijijini kwa sababu huko wengi wao hawajawai kufikiwa na elimu kama hii tunayopatiwa,” amesema Ramadhani
Kuhusu hali ya ulinzi na usalama mkoani Mwanza, kamanda Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi lipo imara na limejipanga vizuri kuhakikisha linawasimamia na kuwaelekeza wananchi na ikiwezekana kuchukua hatua za kisheria kwa watakao fanya uhalifu kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka 2023.