Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui aakizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hali ya malaria huko Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Unguja .
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Na Imani Mtuma, Maelezo
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe Nassor Ahmed Mazrui amewataka wananchi kuimarisha usafi katika maeneo yao ili kuondoa mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria.
Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Unguja amesema endapo jamii itendeleza utamaduni huo itaisaidia serikali kufikia malengo yake ya kumaliza malaria Zanzibar.
Amesama mashirikano ya pamoja kati ya wizara na wananchi ndio njia pekee ya kumaliza maradhi hayo nchini ,hivyo aliwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuondoa vichaka na madimbwi ya maji katika maeneo yao hasa katika kipindi hichi cha mvua ili kupunguza idadi ya wagonjwa na kuondoa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Aidha alisema wizara inaendelea na jitihada za kumaliza ugonjwa huo ikiwemo kupiga dawa majumbani na kutoa vyandarua hivyo aliwataka wananchi kutoa mashirikano wakati wa zoezi hilo na kuendelea kuvitumia vyandarua ili kujikinga na mbu wanaosababisha ugonjwa huo.
Awali alifahamisha kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na muingiliano wa watu katika kipindi cha miezi sita wagonjwa wa malaria wameongezeka sambamba na vifo viwili vilivyosababbishwa na ugonjwa huo.
Alifahamisha kuwa lengo la serikali zote mbili ni kumaliza kabisa ugonjwa huo na kuwataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wizara za Afya juu ya kujikinga na ugonjwa huo ili kushinda vita dhidi ya malaria.