Katika kuadhimisha sherehe za miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amekabidhi bodaboda mbili zenye thamani ya shilingi milioni sita na laki nne kwa makundi ya wasanii na bodaboda ili waweze kutekeleza shughuli zao za kila siku kwa urahisi na kujiongezea kipato
Zoezi la makabidhiano ya pikipiki hizo limefanyika katika viwanja vya CCM Kirumba na kuongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Mhe Michael Masanja Lushinge maarufu Smart ambapo amewataka wasanii na bodaboda waliokabidhiwa pikipiki hizo kuhakikisha wanazitunza na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa
‘.. Nampongeza sana Mhe Mbunge Dkt Mabula hichi alichokifanya hakifanywi na wabunge wa majimbo yote, Yeye amewakumbuka wananchi wake amesikia ombi lenu amewatekelezea tumuunge mkono mkahakikishe zinatumika kama zilivyokusudiwa ..’ Alisema
Aidha Mhe Michael amempongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula Kwa ubunifu wake katika kuanzisha Angeline Jogging Club pamoja na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo
Nae Mbunge Dkt Angeline Mabula amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hasan Kwa fedha nyingi za maendeleo alizozitoa kwaajili ya wananchi wa Jimbo lake kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya sekta ya afya, miundombinu, elimu na kilimo huku akiwaasa wananchi wake kuendelea kumuombea
Bihemo Richard Lukambula ni mwakilishi wa makundi yote ya mbio mkoa wa Mwanza, mbali na kumpongeza Mbunge huyo Kwa kujitoa kwake katika kusaidia jamii na wananchi wake kwa ujumla ametaja faida zitakazopatikana kutokana na kuzinduliwa Kwa The Angeline Jogging Club ikiwemo kuwaweka Vijana pamoja na kushirikishana changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi, kuimarisha afya ya mwili na akili, kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza sanjari kuwaasa Vijana wenzake kuendelea kumuunga mkono mbunge huyo
Viongozi mbalimbali wameshiriki sherehe za maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru akiwemo Katibu tawala wa wilaya ya Ilemela Wakili Mariam Abubakar Msengi, madiwani wa manispaa ya Ilemela, viongozi wa CCM na jumuiya zake wa ngazi za mkoa, wilaya, kata na matawi, vilabu vya mbio vilivyopo mkoa wa Mwanza, wanachama wa CCM na wananchi