Na Mwandishi wetu, Mirerani
Kampuni ya Franone Mining LTD inayomiliki kitalu C machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imetoa msaada wa vyakula vya thamani ya shilingi milioni 31 kwa wahanga waliokumbwa na mafuriko wa Kata za Msitu wa Tembo na Shambarai.
Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD inayomiliki kitalu C, Onesmo Mbise, akizungumza wakati akikabidhi vyakula hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera amesema wametoa msaada huo baada ya kusikia wahanga hao wanahitaji msaada.
Mbise ametaja vyakula hivyo walivyotoa ni magunia 200 ya mahindi, katoni 40 ya mafuta ya kupikia, magunia 40 ya maharage na mifuko 20 ya sukari na vyote vina thamani ya shilingi milioni 31.
“Mheshimiwa DC, sisi kama kampuni ya Franone tunashirikiana na jamii inayotuzunguka ndiyo sababu tuliposikia watu wa Msitu wa Tembo na Shambarai wamepata maafa tukaona tusaidie vyakula hivi,” amesema Mbise.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Hassan Serera, ameishukuru kampuni ya Franone Mining LTD kwa kutoa msaada huo wa wahanga wa mafuriko yaliyotokea eneo hilo.
Dkt Serera amesema japokuwa baadhi ya wahanga nyumba zao zimebomoka kupitia mafuriko hayo na wengine vyakula vyao vimeharibika ila watapata ahueni kupitia msaada huo wa Franone Mining LTD.
“Maeneo yalioathirika mno kwenye wilaya ya Simanjiro ni vijiji vitatu vya Shambarai, Orbili na Kilombero katika kata ya Shambarai na kijiji kimoja cha Londoto kata ya Msitu wa Tembo,” amesema Dkt Serera.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, ameipongeza kampuni ya Franone Mining LTD, kwa kuwachangia waathirika wa mafuriko hayo.
Ole Sendeka amesema Franone Mining LTD imekuwa msaada mkubwa kwa jamii kwani hivi karibuni wakati wa ukame ilisaidia chakula cha shule kwa wanafunzi wa shule mbili za kata ya Naisinyai.
“Franone Mining LTD tunawashukuru kwa mengi, pia mlisaidia shilingi milioni 60 kwa kata za Endiamtu na Naisinyai na mmetumia shilingi milioni 140 kwa jamii hongereni kwa moyo wenu wa kujitolea,” amesema Ole Sendeka.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Asia Ngaliwason ameishukuru kampuni ya Franone Mining LTD na kuahidi kuwa msaada huo utafika kwa wahusika waliokumbwa na mafuriko.
Asia amesema waliokumbwa na mafuriko ni watu 126 na watapata msaada huo katika kata za Shambarai na kata ya Msitu wa Tembo kwenye kaya 49.