WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Twins Auction Mart wakitoa vitu vya wadaiwa sugu katika eneo la Area D jijini Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa opareshini ya kuwaondoa wadaiwa sugu kwenye nyumba za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
ZOEZI likiendelea kwa wadaiwa sugu katika eneo la Area D jijini Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa opareshini ya kuwaondoa wadaiwa sugu kwenye nyumba za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Muonekano wa Nyumba za Wakala wa Majengo (TBA) eneo la Area D jijini Dodoma.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Dodoma, Arch.Vilumba Sanga, akizungumza na waandishi habari wakati wa utekelezaji wa oparesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu kwenye nyumba zake jijini Dodoma .
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Twins Auction Mart, akizungumza na waandishi habari wakati wa utekelezaji wa oparesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu kwenye nyumba za wakala wa Majengo Tanzania (TBA) zilizopo eneo la Area D jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeendeleza opareshini ya kuwaondoa wadaiwa sugu kwenye nyumba zake jijini Dodoma na kupiga marufuku tabia ya baadhi ya wapangaji kuachiana nyumba kiholela bila kufuata utaratibu.
Hayo yamesemwa leo Disemba 8,2023 na Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma, Arch.Vilumba Sanga,wakati akizungumza na waandishi habari wakati wa utekelezaji wa oparesheni hiyo katika eneo la Area D jijini Dodoma.
Arch.Sanga amesema kuwa oparesheni hiyo itakuwa endelevu ili kufanikisha kuwaondoa wadaiwa wote sugu ambao wamelimbikiza madeni ya kodi za pango la nyumba.
Aidha, amesema kuwa wapangaji wanao ondolewa hivi sasa kwenye nyumba hizo ni wale waliolimbikiza madeni kuanzia miezi minne na kuendelea.
“Leo hii tupo hapa kutekeleza oparesheni hii ambayo itakwenda nchi nzia tulianza na Dar es Saalam na leo hii tupo Dodoma lengo ni kuondoa wapangaji wote waachie nyumba mbazo wameshindwa kulipa kodi ili watu wengine waingie.
“Lakini wote ambao wataondolewa na kuonekana kuwa bado wanadaiwa vitu vyao vitashikiliwa na dalali wa Mahaka tuliyeingia mkataba naye ili vipigwe mnada na kufidi deni letu”alisema Sanga
Hata hivyo amesema kuwa oparesheni hiyo ya kuwaondoa wadaiwa hao sugu inatekelezwa na Dalali wa mahakama kampuni ya Twins Auction Mart, ambao ndiyo waliopata zabuni ya kukusanya madeni yote ya TBA.
“Wapangaji ambao tunashughulika nao leo ni wa aina tatu moja ni wale ambao ni wadaiwa sugu na wengine ni wale ambao wameingia kwenye nyumba zetu kinyume na utaratibu kwa kupangishwa kiholela na marafiki zao ambao walikuwa wapangaji wetu awali.
“Kutokana na hali hii kuanazia leo nipige marufuku kwa mtu yeyote kupangishwa nyumba zetu kiholela badala ya kufuata taratibu kwanzia sasa tunaanza kuchunguza na ataye bainika kuingia kwenye nyumba zetu kinyume na utaratibu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”alisema
Aidha Arch.Sanga amewataka V watu wenye mahitaji ya nyumba za kupanga za TBA, kufuata utaratibu uliowekwa badala ya kupangishana kiholela.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Twins Auction Mart, inayotekeleza oparesheni hiyo Zuber Hassan, amesema TBA inadai kiasi cha Sh. bilioni za malimbikizo ya madeni dugu na hadi sasa wameshakusanya kiasi cha Sh. milioni 200 kutoka kwa wadaiwa sugu.