Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo akizungumza na wajumbe wa kamati ya watu wenye ulemavu , kushoto ni Afisa utumishi wa halmashauri Faudhia Nombo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni , Mhe. Daniel Chongolo akiwa katika hafla ya uzinduzi wa kamati ya watu wenyeulemavu wa halmashauri , wa kwanza kushoto ni Afisa utumishi Faudhia Nombo, aliyesimama kulia ni Judithi Kimaro , Afisa ustawi wa jamii ambaye ni katibu wa kamati hiyo.
********************************************
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo ameiasa jamii kutojihusisha na tabia ya kuwanyanyapaa watu wenyeulemavu kwakuwa nawao wanahaki ya kupata hakizote kama ilivyo kwa watu wengine.
Mhe. Chongolo ametoa kauli hiyo leo katika halmashauri ya Kinondoni wakati wa uzinduzi wa kamati ya watu wenye ulemavu ambapo pamoja na mambo mengine amesema ipo dhana iliyojengeka ya kuwanyanya paa watu hao na hivyo kueleza kuwa kufanya hivyo ni makosa na kusisitiza kuwa nilazima itendeke haki na usawa.
Amesisitiza kuwa watu wenye ulemavu wanahaki ya kupewa nafasi mbalimbali na kusema kuwa wote wenye dhamana ya uongozi katika halmashauri hiyo ni lazima kuangalia makundi hayo kwa upekee zaidi kwa kutenda haki na usawa.
Mhe. Chongolo amefafanua kuwa ili kufikia malengo hayo kila mmoja hakuna budi kushirikiana na kamati hiyo iliyoundwa kuweka miundombinu sawia itakayowezesha walemavu kuishi kwa kupata haki zao na usawa pamoja na kuepusha kunyanyapaliwa kama ilivyo kwa sasa.
“ Nawashukuru sana kwakunipa heshima hii ya kuzindua kamati hii ambayo inalenga kusimamia, kushughulikia ipasavyo kutetea haki na usawa wawatu wenye ulemavu” amesema Mhe. Chongolo.
Mhe. Chongolo hakusita kueleza changamoto mbalimbali zilizopo katika halmashauri ya Kinondoni nakusema kuwa sio vijijini tu hata mijini wapo baadhi ya watu wanao wanyanyapaa walemavu kwakuwatenga, kuwaficha pamoja na kuwanyima fursa yakupatiwa huduma kama watu wengine.
“ Jamii imekuwa na taswira mbaya yakuona kwamba ulemavu ni changamoto iliyokuwa na madhara , na hivyo kujikita kunyanyapaa, kamati hii imepewa mamlaka, sasa nendeni mkajenge timu nzuri itakayoleta sura ya kubadilisha mtazamo uliopo hivi sasa na kuleta matunda na faida kwao.
Awali taarifa ya watu wenye ulemavu, ilieleza kuwa halmashauri inajumla ya kata 20 ambazo zinahudumia watu hao wapatao 1239 ambapo kati yao wanaume ni 724 na wanawake 515.
Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa kati ya watu hao wakubwa ni 973 huku watoto wakiwa 266 na kwamba huduma hizo zinatolewa kwakuzingatia sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004, sheria namba 9 ya mwaka 2010 pamoja na mikataba mbalimbali inayohusu watu wenye ulemavu.
Ameeleza kuwa , halmashauri imekuwa ikiviwezesha vyama vya watu wenyeulemavu kwakuvipatia vifaa saidizi kulingana na aina ya ulemavu sambamba na kuwapatia misaada au kujikimu kwa walio na mazingira hatarishi.
Aidha ameeleza kuwa , halmashauri ya Kinondoni imekuwa ikiwaunganisha na asasi za kiraia ili waweze kujipatia ujuzi , ajira na misaada ya kujikumu palipo na uhitaji pamoja na kuwawezesha maadhimisho ya watu wenye ulemavu yanayofanyika kila mwaka.