NA TIGANYA VINCENT
WAKAZI Mkoani Tabora wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za Tabora Green Marathon ambazo ni maalum kwa ajili ya kuhamasisha jamii ili iweze kushiriki katika usafi na utunzaji wa mazingira.
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Tabora Green Marathon.
Alisema mbio hizo zinalenga kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayohimiza usafi na utunzaji wa mazingira kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mwanri alisema wakati wa mbio hizo washiriki watapanda miti katika maeneo mbalimbali na kutangaza vivutio vya utalii ambavyo vinapatikana Mkoani Tabora kwa ajili ya kuwakaribisha wawekezaji katika sekta hiyo.
Naye Mratibu wa Mashindano hayo James Mackanza alisema wao kama wakazi waliopo Manispaa ya Tabora wameamua kuandaa mbio hizo maalumu ili kuunga mkono juhudi za Serikali za upandaji miti na usafi wa mazingira.
Alisema mbio hizo zinatarajiwa kufanyika mwisho mwa Mwezi huu ambapo wamemuomba Mwanamziki Maarufu hapa nchini Ali Kiba kushiriki katika shughuli za kijamii mkoani Tabora siku hiyo na kutoa wito kwa wakazi wa Tabora kujitokeza kujiandikisha ili wapate fursa ya kushiriki na kuweka alama ya utunzaji mazingira mkoani humo.