Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kitama wilayani Tandahimba wakichota maji katika moja ya vituo vilivyojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa wilaya ya Tandahimba.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilayani Tandahimba mkoa wa Mtwara Mhandisi Paulis Nyagali,akiwaonyesha wananchi wa kijiji cha Nannala wilayani humo mabomba yatakayotumika kwenye ujenzi wa mradi wa maji ambao ukikamilika utawezesha kumaliza changamoto ya maji safi na salama katika kijiji hicho.
Tenki linalohudumia wakazi wa kijiji cha Kitama wilayani Tandahimba ambalo ujenzi wake umekamilika.
Na Muhidin Amri,Tandahimba,
WANANCHI wa kijiji cha Kitama wilayani Tandahimba,wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea kero ya huduma ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa zaidi ya miaka 40.
Walisema licha ya kwamba mradi huo umechelewa kukamilika kwa wakati, lakini umeleta faraja kubwa katika maisha yao na uthibitisho mkubwa kwamba Rais Samia ni kiongozi wa wanyonge.
Asha Ahmed alisema,awali walitegemea kupata huduma ya maji kupitia kisima kimoja kilichochimbwa na wafadhili Shirika la maendeleo la nchini Japan(Jaica),lakini kiliharibika na hivyo walilazimika kutumia visima vya asili ambavyo maji yake hayakuwa safi na salama.
Chande Said alisema,kupatatikana kwa mradi wa maji ya bomba uliotekelezwa na Ruwasa ni ukombozi mkubwa kwa kuwa umewaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwenye mito na chem chem za asili.
“mradi huu uliotekelezwa na serikali kupitia wataalam wetu wa Ruwasa ngazi ya wilaya na mkoa, umetusaidia sana sana kumaliza kero ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji mtoni kwa ajili ya matumizi ya kila siku”alisema.
Stamila Fundi alisema,kabla ya mradi huo walilazimika kununua maji kwa gharama kubwa ambapo ndoo moja ya lita 20 iliuzwa kwa Sh.800 hadi 1,000 hali iliyosababisha maisha yao kuwa magumu.
“kwa sasa hatuna shaka kwenye suala la maji,zamani sisi wanawake tuliteseka sana tulikuwa tunatoka nyumbani saa 11 alfajiri na kurudi saa 2 asubuhi na wakati mwingine kutembea umbali zaidi ya kilomita 2 kila siku kwenda kufuata maji hali iliyotusababishia migogoro ya mara kwa mara kwenye ndoa zetu”alisema Stamila.
Afisa mtendaji kata ya Kitama Salome Kapinga alisema,kata hiyo ina vijiji saba,lakini vijiji vinavyopata maji ya bomba ni vitano na vijiji viwili vilivyobaki vinapata maji kutoka kwenye vyanzo vya asili.
Kwa upande wake kaimu meneja wa Ruwasa wilayani Tandahimba Mhandisi Paulis Nyagali alisema,mradi wa maji Kitama kwa sasa unahudumia jumla ya vijiji vitano vyenye wakazi zaidi ya 11,156 baada ya kufanyiwa upanuzi kwa gharama ya Sh.milioni 900.
Amevitaja vijiji vilivyonufaika na mradi huo ni Kitama mjini,Kitama shuleni,Namunda,Mwenge A na Mwenge B ambapo kwa sasa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Aidha alisema,mradi huo umesaidia kupunguza adha kwa wananchi wa vijiji hivyo kutambea zaidi ya kilomita 2 hadi 4 kila siku kwenda kuchota maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Kwa mujibu wa Mhandisi Nyagali,kazi zilitekelezwa katika mradi huo ni kusambaza mtandao wa maji katika vijiji vyote vitano,kujenga vituo 10 vya kuchotea maji,kufikisha huduma ya maji katika taasisi za serikali ikiwemo shule na kituo cha afya.
“sisi kama Ruwasa tumweza kutekeleza mradi huu ambao umekamilika na sasa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kupitia vituo vya kuchotea maji(DPS)na wengine wameingiza maji kwenye nyumba zao”alisema Nyagali.
Katika hatua nyingine Nyagali alisema,Serikali kupitia wizara ya maji imetenga kiasi cha Sh.bilioni 6.5 ili kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa Mkwiti ambao ukikamilika utanufaisha zaidi ya wakazi 26,156 wa vijiji 17 wilayani humo.
Alitaja kazi zinazofanyika ni kujenga vituo 45 vya kuchotea maji,kulaza bomba na kujenga matenki ya kuhifadhi maji na tayari baadhi ya vijiji vimeshaanza kupata huduma ya maji kupitia mradi huo.