Na Sophia Kingimali Dar es Salaam
Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya kusomesha wataalam bingwa na bobezi 601 fani mbalimbali za afya ili kuongeza idadi ya wataalam wenye ujuzi wa kutoa huduma za kibingwa hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo hii Novemba 29, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuongeza wataalam bingwa na bobezi wa afya nchini kwa mwaka wa fedha 2023/24.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya mafunzo ya wataalamu bingwa na bobezi katika fani mbalimbali za Sekta ya Afya ambapo fedha hizo ni muendelelezo wa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema fedha hizo zitatumika kugharamia mafunzo kwa wataalamu wapya 601 sawa na 92% ya waombaji ambao walikidhi vigezo vya kusomea utaalamu wa ubingwa na bobezi wa fani mbalimbali za Sekta ya Afya.
“Ufadhili huu ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo na posho ya utafiti kwa watakaofadhiliwa ndani ya nchi na kwa wanaoenda kusoma vyuo vya nje ya nchi watalipiwa ada, posho ya kujikimu wakiwa masomoni (Stipend), nauli ya kwenda na kurudi pamoja na posho ya utafiti.” Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amewataka wataalamu wote waliopata ufadhili huu wa mwaka 2023/2024 kukamilisha taratibu za kujaza mikataba ya ufadhili kama ishara ya kukubali ufadhili huu.
Amesema kuwa muda wa kujaza mikataba ya ufadhili ni kuanzia tarehe 29 Novemba, 2023 hadi 12 Disemba, 2023 na nakala ya mikataba hiyo inapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Afya na pia itatumwa kwa barua pepe kwenye anuani za barua walizotumia wakati wa kuwasilisha maombi.