NA VICTOR MAKINDA.MOROGORO
Wananachi wa Tarafa ya Mkuyuni, Halmashauri ya Morogoro Mkoani Morogoro, wameepukana na adha ya kukodi magari ya kubebea wagonjwa kwa gharama kubwa kutoka kwa watu binafsi kwa hatua ya serikali kuwapatia gari maalumu la kubebea wagonjwa katika kituo cha afya cha Mkuyuni kinachohudumia wananchi wote wa tarafa ya Mkuyuni.
Wakizungumza kwa furaha kwenye halfa ya kukadhiwa kwa gari hilo la wagonjwa jana, kwenye kituo hicho cha afya, wananchi hao walimpongeza mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mshariki, Hamis Taletele na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwaptia gari hilo la wagonjwa ambapo walisema kuwa litaleta ukombozi mkubwa kwao kwa kuwa walikuwa wakilazimika kukodi magari kwa watu binafsi kwa fedha nyingi pindi wagonjwa wao wanapopata rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro iliyo umbali wa Kilometa 35.
“ Hapa kwenye kituo chetu cha afya tunapata huduma nzuri za matibabu na hata operesheni za uzazi zinafanyika, lakini tunapopewa rufaa kwenda hospitali ya mkoa, kwa kweli tulikuwa tunateseka sana hasa sisi akina mama na watoto”. Alisema Zainabu.
Zainabu aliongeza kuwa kupatikana kwa gari hilo la wagonjwa kutakuwa ni ukombozi kwa wananchi wa Tarafa hiyo wanaohudumiwa katika kituo hicho cha afya kwa kuwa awali walilazimika kukodi magari ya watu binafsi, ambapo ilikuwa ikiwagharimu pesa nyingi.
Akizungumza wakati wa halfa ya kukabidhi gari hilo la wagonjwa, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Msahariki, Hamis Taletele, alisema kuwa gari hilo ni miongoni mwa ahadi zake alizozitoa kwa wananchi wa Tarafa ya Mkuyuni kuwa angeliwapatia gari la wagonjwa kwenye kituo hicho cha afya ili liweze kuwa msaada kwao pindi wanapopata rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.
“ Niliwaahidi kuwa kabla sijamaliza kipindi changu cha miaka mitano ya ubunge, nitahakikisha wananchi wa Mkuyuni mnapata gari ya wagonjwa kwenye kituo chenu cha afya, leo ninatekeleza ahadi yangu, nimepambana serikali yenu ya CCM imewapatia gari hilo. Alisema Taletale.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro, Lukas Lemomo akizungumza katika halfa ya makabidhiano ya gari hilo la wagonjwa, aliutaka uongozi wa kituo cha Afya Mkuyuni, kulitunza gari hilo sambamba na kulitumia kwa malengo mahususi.